Na Mwandishi Wetu,TimesMajira online
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya,Maendeleo Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Profesa Abel Makubi amesema kuwa magonjwa yasiyoambukiza yanaendelea kuathiri jamii na yanachangia idadi ya vifo asilimia 40 hadi 45 kwa sasa ikilinganishwa na na asilimia 33 kwa miaka mitano iliyopita.
Profesa Makubi ameyasema hayo katika taarifa yake iliyotumwa kwa vyombo vya habari hivi karibuni ambapo alisema kuwa magonjwa hayo ni pamoja na Saratani, Kisukari, Shinikizo la damu na mengineyo ambapo serikali inaendelea kuwakumbusha wananchi kuchukua tahathari za kujikinga nayo kwa kufanya mazoezi, kupunguza vyakula vya mafuta, pombe, chumvi nyingi, kuepuka unene pamoja na kuacha kuvuta sigara.
Ameeleza kuwa wanahimiza tabia hizo za kujikinga zijengwe kuanzia ngazi ya familia na mashuleni ili kuwakinga watoto pamoja na kuwapa mwamko wa kujikinga wakiwa katika umri mdogo na kuweza kuepuka madhara yatayowza kutokea hapo baadae.
Aidha amefafanua kuhusiana na ugonjwa wa UKIMWI amesema kuwa ugonjwa huo umeendelea kupungua kwa asilimia 4.7 huku idadi ya vifo ikipungua kwa asilimia 48 kutoka mwaka 2015 ambapo kwa upande wa ugonjwa kifua kikuu maambukizi yamepungua kwa asilimia 23 na vifo vikipungua kwa asilimia 33 kwa kipindi cha miaka 3 iliyopita.
“Kwa ugonjwa wa Malaria vifo vimepungua kwa zaidi ya asilimia 60 kati ya mwaka 2015 na mwaka 2020 na kutokana na takwimu hizi utaona kuwa Tanzania imepiga hatua katika mapambano dhidi ya magonjwa mbalimbali lakini bado tunatakiwa kukumbushana juu ya mbinu za kujikinga,” amesema Profesa Makubi.
Ameendelea kusema kuwa kwa upande wa vita dhidi ya magonjwa ya mlipuko inaendelea na wizara inawakumbusha wananchi kuzingatia taadhari iliyotolewa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu kuwa watanzania waendelee kuchukua taadhari ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa COVID 19 ambapo kwa hali ya Tanzania hadi hivi sasa serikali imeweza kuudhibiti ugonjwa huo kwa kiasi kikubwa na kuepusha athari kubwa.
“Kutokana na hali ya ugonjwa huu katika mataifa mengine tunapenda kuelimisha na kufafanua tena juu ya mambo muhimu ya kuzingatia katika kujikinga ambapo ni pamoja na kuondoa hofu, kunawa mikono mara kwa mara, kuvaa barakoa panapo lazimika, kufanya mazoezi, pamoja na kula lishe bora,” ameeleza.
Sambamba na hayo pia ametoa wito kwa wananchi kutambua afya zao na kujilinga hasa makundi maalum ya wazee, watu wenye uzito mkubwa, wenye magonjwa sugu kama vile pumu,shinikizo la damu, Kisukari, Moyo na Figo ikiwa ni pamoja kuwahi katika vituo vya afya mara mtu anapoona dalili za maradhi pamoja na kutokusahau tiba za asili za kunywa na kujifukiza zizosajiliwa na Baraza la tiba asili.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi