Na Hadija Babasha, TimesMajira Online
CHAMA cha Wananchi CUF kimesema killikuwa na matarajio makubwa kwamba mazungumzo ya Rais Samia Suluhu Hassan na na vyama vya siasa yatafanyika mapema kama alivyoahidi baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM, lakini hadi sasa bado hajatimiza ahadi hiyo.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema, hadi sasa Rais Samia hajakutana na viongozi wa vyama vya siasa licha ya kwamba baadhi yao walikubali mialiko ya kwenda Dodoma wakati alipohotubia Taifa.
Profesa Lipumba amesema, Rais aliahidi kukutana na vyama vya siasa kwa ajili ya kuzungumzia hali ya demokrasia nchini, lakini hajatimiza ahadi hiyo hadi sasa.
“Bila shaka agenda kuu ya mazungumzo yake na vyama vya siasa itakuwa kukamilisha zoezi la kupata katiba mpya inayotokana na maoni ya wananchi kama yalivyoratibiwa na Tume ya Jaji Warioba, ndani ya rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba kuna misingi na mfumo wa namna ya kupata Tume Huru ya Uchaguzi,” amesisiza Prof.Lipumba.
Profesa Lipumba ametumia nafasi hiyo kumuomba Rais Samia kulipa kipaumbele suala la katiba mpya akiamini itasaidia kulinda uchumi atakaoujenga katika kipindi chake cha uongozi.
Amesikitishwa na kauli ya Rais Samia aliyoitoa wiki iliyopita wakati wa mkutano na wahariri wa vyombo vya habari kwamba suala la Katiba Mpya lisubiri ajenge uchumi kwanza.
Profesa Lipumba amesema CUF wanaamini Katiba na uchumi ni vitu vinavyotakiwa kwenda pamoja.
“Tanzania tumekuwa tukiambiwa tumefikia uchumi wa kati, sasa anataka tufikie uchumi wa juu ndipo tushughulikie suala la katiba? Amehoji Profesa Lipumba.
Mbali na hilo, Profesa Lipumba amemshauri Rais Samia kujiwekea malengo binafsi ya kuchukua tuzo za MO IBRAHIM ambayo hutolewa kwa viongozi walioongoza vizuri hasa katika suala zima la demokrasia, kupambana na ufisadi na kupunguza umasikini kwa wananchi wao na kutokusubiri mpaka wananchi waandamane kudai katiba.
Profesa Lipumba ameeleza kuwa, demokrasia ni nyenzo bora ya kujenga uchumi Shirikishi na Katiba ni hitaji la misingi kwa wananchi kuliko kuwa maslahi binafsi kwa wanasiasa.
Hivyo amemuomba Rais Samia kumaliza mchakato huo ulioanza katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne.
Akizungumzia kuhusu mikutano ya vyama vya siasa, Profesa Lipumba amesema kuwa, katika uongozi wa Rais John Magufuli uhuru wa kikatiba na kisheria wa vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara ulizuiliwa, hivyo sera hiyo haikuongeza uwekezaji kutoka nje.
Amesema Katiba iliyopo sasa haimpi mamlaka Rais kuzuia mikutano ya vyama vya siasa na kwamba kufanya hivyo ni kinyume cha matakwa ya sheria na kumsihi Rais Samia kutimiza ahadi yake ya kukutana na viongozi wa vyama vya siasa nchini.
Hata hivyo Profesa Lipumba amesema serikali imefanya jambo jema kuwaaachia huru Mashekh wa Uamsho wa Zanzibar waliokaa jela kwa zaidi ya miaka minane.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi