December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Kitila:Miaka 60 ya muungano nchi inajivunia kutatua changamoto zilizojitokeza

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline Dodoma

WAZIRI wa Mipango na Uwekezaji Prof.Kitila Mkumbo amesema kuelekea miaka 60 ya Muungano nchi inamengi ya kujivunia ikiwemo mafanikio ya kuzikabili na kuzitatua changamoto zilizojitokeza.

Prof.Mkumbo amesema hayo jijini hapa leo,Aprili 17,2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika miaka 60 ya Muungano ambapo amesema Serikali imejidhatiti kupambana na changamoto zitakazojitokeza ambazo zitatishia muungano.

“Tunapopima mafanikio kama nchi, tunazungumzia uhai wa taifa na Sisi kama taifa hatua ya kwanza ya kujipima katika miaka 60 ya muungano ni uhai wa muungano wetu,”amesema Pro.Kitila.

Amesema kitu kingine cha msingi kama nchi,ilipanga kupambana kuhakikisha kwamba muungano huo unadumu na ilipanga kulinda amani, utulivu na mshikamano ambapo hayo yote yamefanikiwa.

Amesema kuwa hatua ya kwanza kujipima katika maendeleo ni kuwa na usalama wa chakula wakati wa muungano usalama wa chakula ulikuwa asilimia 60 huku lengo la nchi ni kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 100 na kuwa na akiba kwa sasa nchi ina usalama wa chakula kwa asilimia 124.

Ametaja hatua ya pili ambayo amesema kujipima katika maendeleo ni ustawi wa watu na nchi kwa kuangalia mambo ya msingi ya kibinadamu ikiwemo chakula, mavazi na malazi ambayo nayo imepigwa hatua kubwa.

Aidha amesema wakati nchi inapata Uhuru, umri wa kuishi kwa Mtanzania ilikuwa wastani wa miaka 32, mwaka 2000 umri wa kuishi ukasogea hadi wastani wa miaka 52.

“Tamaa yetu ifikapo mwaka kesho 2025 wastani wa kuishi uwe miaka 68 Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, wastani wa kuishi ni miaka 66,”amesema.

Vilevile ameeleza kuwa mambo matatu ya kufanya kukuza ustawi wa binadamu ni kumpa binadamu elimu ili aweze kuishi vizuri ambapo mwaka 2000 nchini Tanzania, kiwango cha kuandikisha wanafunzi kilikuwa asilimia 69 Kwa malengo tuliyojiwekea kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025, ni kufikia asilimia 100 ya uandikishaji wa wanafunzi ambapo hadi sasa nchi imevuka malengo,hadi asilimia 108.5.

Amesema kuhusu suala la kwenda sekondari, mnamo mwaka 1964 ilikuwa asilimia 5, mnamo mwaka 2000, watoto waliofanikiwa kufika sekondari kutoka shule za msingi ilikuwa chini ya asilimia 20 ambapo amesema lengo ifikapo mwaka 2025,nchi iwe imefikia asilimia 48 Kwa takwimu za hivi sasa,ipo asilimia 70.

“Dira ya Maendeleo ya Taifa inayokuja, tutahitaji elimu ya msingi Tanzania iwe kwa Watanzania wote lazima kufika sekondari kwa asilimia 100,”amesema.

Ametaja eneo la pili la kukuza ustawi wa binadamu ni afya hasa kwenye eneo la mama na mtoto, na la tatu ni maji ambapo wakati nchi inapata uhuru, uwepo wa maji vijijini ulikuwa chini ya asilimia 15 na mwaka 2000 ilikuwa asilimia 32 Kwa sasa ni asilimia 77.