November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof. Gurnah awasili nchini kushiriki Tuzo ya Taifa ya Uandishi Bunifu

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online DSM

MWANDISHI Mkongwe wa vitabu Prof. Abdulrazak Gurnah ametua nchini Tanzania tayari kwa tukio la tuzo ya Taifa ya uandishi Bunifu ambayo itafanyika Aprili 13, 2024 katika ukumbi wa The Super Dom uliopo Masaki Jijini Dar es Salaam.

Prof. Gurnah anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika usiku wa tuzo hiyo ambayo inaratibiwa na Taasisi ya Elimu Tanzania chini ya uangalizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, na hufanyika Aprili 13 ikiwa ni kumbukizi ya siku ya kuzaliwa ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, katika uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Prof. Gurnah ameeleza; “Ni heshima kubwa kualikwa kuja kuungana katika sherehe hii ya tuzo ya kimataifa ya Mwl. Nverere ili kuwasaidia waandishi wenzangu, lakini pia kuja nyumbani kuonana na wenzangu ndugu na jamaa.’’ Amesema Prof. Gurnah.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amemshukuru Prof. Gurnah kwa kukubali mwaliko huo kwani ni heshima ya kipekee kwa washiriki wabunifu wa tuzo hizo kukutana na mwandishi huyo nguli.

Katika tukio hilo la mapokezi Prof. Mkenda aliambatana na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt. Aneth Komba aliyeambatana na watumishi mbalimbali kutoka Taasisi hiyo.