January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Elisante atoa wito kwa wananchi,watendaji wa mahakama kujitokeza kuboresha taarifa zao

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

MTENDAJI Mkuu wa Mahakama Prof.Elisante Ole Gabriel ametoa wito kwa wananchi wote  pamoja na watumishi wa Ofisi yake mkoani Dodoma kujitokeza kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la mpiga kura ili kuweza kupiga kura wakati wa uchaguzi.

Prof.Ole Gabriel amesema hayo jijini hapa leo Septemba 25,2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuboresha taarifa zake kwenye daftari la kudumu la Mpiga kura katika kituo cha uandikishaji cha Damu Salama,Mtaa wa Tambukareli,kata ya Hazina.

Amesema kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imefanya vizuri katika zoezi hilo kwani mtu hana haja ya kwenda alikojiandikishia bali anaboresha taarifa zake alipo sasa na anapoweza kupiga kura na mifumo ya TEHAMA inamtambua hivyo imerahisisha kwa kila aliyefikia umri wa kupiga kura na tayari wenyevitambulisho vya mpiga kura kwenda kuboresha taarifa zao.

“Hili zoezi ni la kidigitali kwani mashine zinaweza kufanyakazi kwa mfumo wa betri hivyo hata sehemu ambazo hazina umeme zinaweza kufanyakazi.

“Lakini mimi nipo katika Mahakama na tunatumia mifumo ya TEHAMA na unaweza ukaingia kwenye mfumo ukaingiza taarifa zako halafu ukafika hapa ikawa rahisi zaidi kwasababu zitaonekana na hawa wenzetu wameweka namna ambayo mtu hawezi kujiboreshea mwenyewe moja kwa moja hadi afike kwenye vituo vya uandikishaki ili wasiweze kuruhusu wageni kujiandikisha,”amesema Prof.Ole Gabriel.

“Hivyo nitoe wito kwa wananchi wote wa Dodoma wajitokeze kwani zoezi ni la muda mfupi tu mimi nimetumia dakika tano na sekunde sita tu.

“Watumishi wenzangu wa Mahakama mjitokeze kuboresha taarifa zenu hii haisiani na dini wala Chama kwani kupiga kura ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu,”amesema.