Na Mwandishi Wetu, TimesMajira online
Timu ya Maafande wa Tanzania Prisons jana imeshindwa kutamba katika uwanja wake wa nyumbani wa Nelson Mandela baada ya kulazimishwa sare ya goli 2-2 na Wagosi wa Kaya, Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL).
Hii ni mara ya pili timu hizo zinagawana pointi moja ndani ya msimu huu baada ya Desemba 13 kugawana alama moja katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliomalizika kwa suluhu ya bila kufungana.
Katika mchezo huo, wenyeji Prisons walikuwa wa kwnza kupata goli lililofungwa dakika ya 19 na Samson Mbangula aliyetumia vema makosa ya kipa Abubakar Abasi aliyetoka golini lakini dakika nne baadaye Coastal walisawazisha kwa mkwaju wa penalti iliyopigwa na Abdul Suleiman baada ya mchezaji wao Prisons kuunawa mpira ndani ya 18.
Dakika ya 36, Prisons walipata goli la pili lililofungwa na Jeremiah Juma ambalo ni goli lake la saba ndani ya msimu huu na kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa goli 2-1.
Kipindi cha pili, Coastal waliingia kusaka goli la kusawazisha ambapo dakika ya 85 Mudathir Said aliisawazishia Coastal na mchezo huo kumalizika kwa sare ya goli 2-2.
Licha ya matokeo hayo kuwasogeza Prisons hadi nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi baada ya kufikisha pointi 42 lakini hali si swari kwa Coastal ambao wameendelea kusalia katika nafasi ya 16 wakiwa na pointi zao 34.
Sasa timu hiyo inahamishia nguvu katika mechi zao tatu zilizosalia msimu huu dhidi ya Simba, Mwadui na Kagera ambazo wanahitaji kushinda ili kusaliz Ligi Kuu msimu ujao.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania