Na Joyce Kasiki, Dodoma
MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imezindua filamu iitwayo “Winga” ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu fursa zilizopo katika ununuzi wa umma.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa PPRA, Remija Salvatory, amesema mamlaka hiyo imeamua kutumia filamu kama njia mbadala ya kufikisha ujumbe kwa kundi kubwa la watu wanaopenda kuangalia filamu, ili waweze kutambua na kuchambua fursa za zabuni za serikali kwa urahisi kama wanavyopata burudani nyingine.
Amesema filamu hiyo inaonesha wazi kuwa katika ununuzi wa umma unaofanyika kupitia mfumo wa NeST (National e-Procurement System of Tanzania) hakuna mtu wa kati, kwani mfumo huo ndio njia pekee ya kuunganisha wazabuni na fursa za manunuzi ya serikali.
Aidha, viongozi wa PPRA wamefafanua kuwa filamu ya “Winga” imebeba maudhui yanayoonesha safari ya mhusika mkuu anayejifunza namna ya kutumia mfumo wa NeST hatua kwa hatua hadi kufanikiwa kushiriki zabuni kwa kufuata taratibu zote. Kupitia simulizi hiyo, watazamaji wanapata ufahamu wa vitendo kuhusu usajili, uwasilishaji wa nyaraka na ufuatiliaji wa matangazo ya zabuni.
Amesema ,filamu hiyo pia inalenga kuondoa dhana potofu miongoni mwa baadhi ya wananchi kuwa mchakato wa zabuni za serikali ni mgumu au unahitaji kujuana. Kupitia elimu inayotolewa, PPRA inasisitiza kuwa mfumo wa NeST umejengwa katika misingi ya uwazi, ushindani wa haki na usawa kwa wazabuni wote.
Katika hatua nyingine, mamlaka hiyo imeeleza kuwa itaendelea kutumia mbinu mbalimbali za mawasiliano ikiwemo mitandao ya kijamii, vipindi vya redio na televisheni pamoja na makongamano ya wadau ili kuhakikisha elimu kuhusu ununuzi wa umma inawafikia wananchi wengi zaidi, hususan vijana na wajasiriamali wadogo wanaotaka kushiriki katika zabuni za serikali.
Kwa upande wao, baadhi ya wadau walioshiriki uzinduzi wa filamu hiyo wamesema kuwa matumizi ya filamu kama chombo cha mawasiliano yatawasaidia watu wengi kukumbuka ujumbe huo na kufikia makundi ambayo mara nyingi yanaonekana kuwa mbali na fursa za manunuzi ya umma.
Wamesema hatua hiyo itasaidia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kushiriki katika zabuni za serikali kupitia mifumo rasmi.

More Stories
Kihongosi amtaka mkandarasi kuwalipa vibarua stahiki zao
DC Mbozi afuturisha wananchi, asisitiza mshikamano na Umoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Nina imani mubna utendaji kazi wa ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria