March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PPRA, VETA waanzisha ushirikiano mpya kuongeza ushiriki wa makundi maalum kwenye zabuni za serikali

Na Joyce Kasiki,Dodoma

MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeingia makubaliano ya ushirikiano na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) unaolenga kutekeleza matakwa ya sheria mpya ya ununuzi inayozitaka taasisi za serikali kutenga angalau asilimia 30 ya miradi kwa makundi maalum.

Akizungumza baada ya utiaji saini Novemba 20,2025,Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dkt. Denis Simba, alibainisha kuwa bado kuna changamoto ya ushiriki mdogo wa makundi haya kutokana na ukosefu wa elimu ya taratibu, namna ya kujisajili na jinsi ya kuingia kwenye mifumo rasmi ya serikali.

 “Maelfu wanastahili kunufaika na asilimia 30 ya zabuni, lakini wengi hawana uelewa wa hatua za kuingia kwenye mfumo. Makubaliano haya ni daraja la kuongeza elimu, usajili na ushiriki wao,” alisema Dkt. Simba.

Aidha alisema hadi sasa, PPRA imeeleza kuwa ni vikundi takribani 1,000 tu vilivyosajiliwa kwenye mfumo wa NEST, vikiwa na thamani ya miradi inayozidi shilingi bilioni 30kiwango ambacho ni kidogo ikilinganishwa na lengo la kufikia trilioni 5 na kuwahusisha zaidi ya wananchi milioni 3.

Kwa mujibu wa Dkt.Simba alisema mpango huu unatarajiwa kuongeza ajira, kuimarisha ujuzi na kuchangia ukuaji wa uchumi kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Antony Kasory, alisema makubaliano hayo yatawapa nafasi wahitimu kutoka makundi maalum kupata fursa za moja kwa moja kwenye miradi ya serikali baada ya kusajiliwa kwenye mifumo ya ununuzi.

“Katika kila wilaya tuna wahitimu kutoka makundi maalum. Kupitia ushirikiano huu, tutajenga uwezo wao na kuhakikisha wanajisajili kwenye mifumo ya serikali ili ujuzi wao utekelezwe kwenye miradi halisi,” alisema CPA Kasory.

Aidha imeelezwa kuwa  makubaliano hayo, VETA imepanga kufikisha elimu kwa kila wilaya ili kuongeza uelewa wa taratibu za usajili, huku PPRA ikishirikiana na taasisi nunuzi kupanua idadi ya vikundi vitakavyonufaika na asilimia 30 ya zabuni.