February 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PPAA yazuia zabuni zenye thamani ya bilioni 583

Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza

Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imefanikiwa kuzuia utoaji wa tuzo kwa zabuni 35, zenye thamani ya zaidi ya bilioni 583,tangu Machi 2021  mpaka sasa.

 Zabuni hizo zilikuwa na wazabuni wasio na uwezo wa kifedha na wale waliokosa sifa za kitaalamu za kutekeleza zabuni husika. Hatua hii imeepusha Serikali kuingia katika mikataba itakayosababisha  utekelezaji wa miradi isioridhisha, kusababisha  upotevu wa fedha za umma na kuchelewesha maendeleo stahiki kwa wananchi.

Hayo yamebainishwa Februari 4,2025, na Katibu Mtendaji wa PPAA,James Sando, katika ufunguzi wa mafunzo  ya moduli ya kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektoniki yalioambatana na tamko rasmi la kuanza kwa matumizi ya moduli kupitia mfumo wa NeST,ambayo yanafanyika kwa siku tatu mkoani Mwanza na kuhusisha washiriki kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa.

“Tangu  Serikali  ya awamu ya sita ilivyoingia madarakani mpaka sasa, Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma(PPAA),imefanikiwa kushughulikia mashauri 162, yaliotokana na michakato mbalimbali ya ununuzi wa umma.

Kati ya mashauri hayo ilizuia utoaji tuzo kwa zabuni 35, zenye thamani ya zaidi ya bilioni 583,kwa wazabuni wasio na uwezo wa kifedha pamoja na wale waliokosa sifa 

za kitaalamu za kutekeleza zabuni husik,”amesema Sando.

Sando,ameeleza kuwa PPAA kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na taasisi nyingine zinazoshughulikia ununuzi wa umma, imefanikisha kutungwa kwa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya 2023 na Kanuni za Ununuzi za 2024.

 Sheria hiyo,ilioanza kutumika Juni 2024 na kanuni zake,imeleta maboresha  katika eneo la ununuzi na ugavi ikiwemo kupunguza muda wa

kushughulikia malalamiko na rufaa zinazotokana na michakato ya ununuzi wa umma.

Kwa mfano, muda wa kuwasilisha malalamiko kwa taasisi nunuzi umepunguzwa kutoka siku saba hadi siku tano za kazi, na muda wa PPAA kushughulikia rufaa umepunguzwa kutoka siku 45 hadi siku 40. Hii ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha ufanisi na uwazi katika michakato ya ununuzi wa umma.

Aidha, Sando aliiomba Serikali kiasi cha bilioni 5 hadi 7 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za PPAA katika eneo la NCC Link, mkoani Dodoma.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha,Dkt.Mwigulu Nchemba, Kamishina wa Sera za Ununuzi wa Umma, Dkt. Frederick Mwakibinga, alisisitiza faida za kutumia moduli ya kielektroniki, kuwa inasaidia kupunguza muda na gharama, kuongeza uwazi na kupambana na rushwa. 

Pia Aliwaasa wazabuni na taasisi nunuzi kuwa tayari kutumia mfumo huo ili kurahisisha uwasilishaji na usimamizi wa malalamiko na rufaa.

Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Godfrey Mbanyi, aliongeza kuwa lengo la Serikali ni kupunguza migogoro katika mchakato wa ununuzi wa umma. Alisisitiza ushirikiano wa maofisa ununuzi, wazabuni, na maofisa masuuli ili kuhakikisha michakato ya ununuzi inakuwa ya haki na inajali maslahi ya taifa.

Kwa kumalizia, alikumbusha kuwa upotevu wa fedha katika mchakato wa ununuzi haungalii maeneo fulani tu, bali unahusisha maslahi ya taifa zima, hivyo ni muhimu kwa kila mtendaji kufuata sheria na kufanya kazi kwa maadili.

“Fedha ikipotea Mwanza,siyo ya watu wa Mwanza ni ya Tanzania yote,Nikipata changamoto ya kiafya nikiwa Mwanza nitaenda hospitali iliopo hapa,nikikosa huduma kwa sababu ya fedha ya kununua dawa iliochezewa kiujanja ujanja maana yake umeniathiri mimi ingawa siyo Mkazi wa Mwanza,”.