January 18, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi yatoa matibabu na ushauri wa kiafya kwa wazee

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Jeshi la Polisi la Mkoa wa Arusha limetoa huduma ya matibabu na ushauri wa kiafya katika kituo cha AST maalumu kwa ajili ya kuwalea wazee wanaoishi katika mazingira magumu Jijini Arusha.

Mwenyekiti wa mtandao wa Polisi wanawake Mkoa wa Arusha (TPF NET) Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP MARY KIPESHA amebainisha kuwa kupitia mtandao huo wametoa msaada wa vitu mbalimbali pamoja na huduma ya kiafya ikiwa mwendelezo wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia mkoani humo.

ACP Kipesha amesema mbali na kutoa msaada huo, katika siku hizo 16 za kupinga ukatili amebainisha kuwa wametoa elimu katika shule, hospitali, nyumba za ibada, masoko pamoja na stendi za mabasi ambapo jamii imepata uelewa wa kutosha.

Mkurugenzi wa Kituo hicho Bi. Ester Njau amelishukuru Jeshi hilo kwa kutoa matibabu kwa wazee wanaoishi katika kituo hicho ambapo amebainisha kuwa matibabu hayo pamoja na vitu mbalimbali vilivyotolewa vitaboresha afya za wazee hao.

Naye Bi. Mary Wakati akisoma risala amesema kuwa awali walifanya uchunguzi na kubaini kuwa wazee wengi maeneo mbalimbali katika mkoa wa Arusha wanakabiliwa na mazingira magumu ya kuishi pamoja na jamii kushindwa kutambua uwepo wa wazee na kushindwa kuwahudumia.

Aidha Bi. Regina Eusebi kwa niaba ya wazee wenzake mbali na kushukuru Jeshi la Polisi kwa msaada walioutoa ametoa wito kwa makundi mengine kutoa misaada katika vituo vinavyolea watu wenye uhitaji mbalimbali.

Kwa upande wa Diwani wa Kata ya Elerai Bwana Losioki laizer ameshukuru Jeshi la Polisi kwa kuwajali wazee wanaoishi katika mazingira magumu na kutoa wito kwa makundi mengine kuiga mfano ulioneshwa na Jeshi hilo wa kujali wazee.