December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi yakabidhi vifaa kikundi shirikishi cha ulinzi Ifumbo

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

KAMANDA wa polisi Mkoani Mbeya Kamshina msaidizi wa polisi, Benjamin Kuzaga amekabidhi vitendea kazi vya kisasa ambazo ni radio redio za mawasiliano (radio calls) kwa kikundi cha ulinzi shirikishi cha kata ya Ifumbo wilayani Chunya mkoani hapa ili kuweza kuzuia uharifu katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo .

Kamanda Kuzaga amesema hayo Januari 29, mwaka 2024 katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo kwa kikundi hicho ambacho kimekuwa kikijishughulisha na ulinzi shirikishi.

Aidha Kuzaga amesema amekemea vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kuwafichua watu wanaofanya Matukio hayo ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mwekezaji ambaye pia ni mmiliki wa kampuni ya G&I inayojishughulisha na uchimbaji madini , Selemani Kaniki amesema kuwa, Kata ya Ifumbo inakwenda kulindwa kidigitali kupitia mifumo ya kisasa ya mawasiliano.

“Niliona mbali sana, wananchi wa kata ya Ifumbo wamekuwa wa kwanza kuwa na kikundi cha ulinzi shirikishi kinachotumia redio za mawasiliano (radio calls) kufanya shughuli za ulinzi, nenda popote hutokuta kitu hiki” amesema Kaniki.

Aidha ameongeza kuwa, matumizi ya redio za mawasiliano yanakwenda kuleta ufanisi katika ulinzi wa Kata ya Ifumbo pamoja na vijiji jirani kwani redio hizo zina uwezo wa kushika mawimbi zaidi ya umbali wa kilomita kumi hivyo zimekuja kutatua changamoto za kimawasiliano.

Naye mkazi wa Kata ya Ifumbo ,Charles Mkomolo amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kupeleka Mkaguzi Kata pamoja na kuhimiza na kuhamasisha vikundi vya ulinzi shirikishi hali inayopelekea kuimarika kwa ulinzi na usalama wa wananchi wa Kata hiyo.

Mbali na kutoa vifaa vya ulinzi, Mwekezaji Kaniki ameahidi kujenga kituo cha Polisi Kata ya Ifumbo ili kutatua changamoto ya kutembea umbali wa zaidi ya kilomita zaidi ya 45 hadi kituo cha Polisi Chunya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ACP Benjamin Kuzaga kupitia hafla hiyo amekabidhi ramani ya kituo cha Polisi kwa uongozi wa Serikali Kata ya Ifumbo ili kuanza maandalizi ya ujenzi wa kituo hicho ikiwa ni pamoja na kutoa eneo la mradi wa ujenzi.