January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ACP. Muliro Jumanne

Polisi wafanikiwa kuzuia wizi benki

Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza limefanikiwa kuzuia tukio la uhalifu wa ujambazi/wizi katika benki ya CRDB tawi la Igoma Wilayani Nyamagana Mkoani hapa.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia leo Julai 5 saa nane usiku katika benki hiyo baada ya kundi la wahalifu wanaosadikiwa ni majambazi kuvunja eneo la nyuma la jengo la benki hiyo ambayo imepakana na majengo mengine na kufanikiwa kukata paa na dari (ceiling board) na kupata mwanya wa kuingia ndani ya benki hiyo.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusiana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ACP. Muliro Jumanne amesema, Polisi waliokuwa lindo katika eneo hilo walibaini kuwepo kwa mazingira yasiyo ya kawaida na walipozungukia jengo hilo kwa ajili ya kufanya uchunguzi kwa kina walibaini kuwepo kwa mmoja wa majambazi aliyekuwa tayari ndani akijaribu kutoka kupitia sehemu waliovunja wakati wa kuingia.

“Askari walimuamuru ajisalimishe lakini alikaidi amri hiyo halali na walimrushia risasi iliomjeruhi mkono na bega la kulia na kulazimika kurudi ndani ya benki na akakamatwa huku akiwa katika hali mbaya,” amesema ACP.Muliro.

Amesema, mtuhumiwa alikimbizwa hospitali ya Mkoa ya Sekou-Toure kwa matibabu lakini kwa bahati mbaya alifariki akiwa bado yupo njiani hivyo mwili wa marehemu umeifadhiwa hospitalini hapo kwa kusubiri uchunguzi wa daktari na utambuzi.

Pia amesema, uchunguzi wa awali uliofanyika eneo la tukio kwa kushirikiana na Meneja wa benki hiyo umebaini kuwa licha ya wahalifu hao kuingia ndani ya benki na kuvuruga droo za ofisi hizo lakini hawakuweza kufanikiwa kuiba fedha zilizokuwa zimeifadhiwa sehemu maalumu.

Aidha ameahidi Jeshi hilo kuendelea na ufuatiliaji mkali wa kuhakikisha watuhumiwa wengine walioshiriki kupanga na kujaribu kutenda tukio hilo wanakamatwa.

Hata hivyo amesema jeshi hilo linaendelea kutoa onyo kali kwa baadhi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kutojaribu au kufanya vitendo hivyo kwani hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kukamatwa zitachukuliwa dhidi yao.

“Kitendo kilichofanywa na mhalifu huyu ambaye sasa ni marehemu licha ya kuwa ni kosa kisheria lakini ni dharau na kejeli kwa jeshi letu ambalo limeapa kutovumilia vitendo vya namna hii,” amesema ACP. Muliro.