December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wachezaji wa Biashara United Mara wenye jezi nyeupe wakimenyana na Polisi Tanzania wenye jezi za bluu katika dimba la Karume Mjini Musoma. (Picha na Fresha Kinasa)

Polisi Tanzania waichapa Biashara United nyumbani

Na Fresha Kinasa,TimesMajira Online, Mara

Timu ya Polisi Tanzania kutoka mkoani Kilimanjaro imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Timu ya Biashara United Mara katika mchezo wake wa ugenini uliochezwa katika dimba la kumbukumbu ya Karume mjini Musoma mkoani Mara.

Katika mchezo huo, timu zote zilienda mapumziko bila kufungana kutokana na washambuliaji wa pande zote mbili kupata nafasi kadhaa lakini, wakashindwa kuzitumia kutokana na uhodari wa walinzi wa timu zote mbili.

Gari la Polisi likiwa limeimarisha ulinzi kwa basi la wachezaji wa Polisi Tanzania wakati likiondoka uwanjani. ( Picha na Fresha Kinasa).

Bao la Polisi Tanzanaia liliwekwa kimiani na mshambuliaji Erick Msagati katika dakika ya 50 ya kipindi cha pili baada ya kupiga mpira uliokwenda moja kwa moja langoni na kumshinda mlinda mlango wa Biashara United Mara, Daniel Mgole.

Mchezo uliendelea kwa kasi kubwa huku Biashara United Mara wakitafuta bao la kusawazisha na timu ya Polisi Tanzanaia wakitafuta kuongeza bao, lakini mpaka mwisho wa mtanange huo bao hilo liliweza kudumu.

Kocha wa Biashara United Mara, Francis Baraza amesema majeruhi kwa baadhi ya wachezaji wake imechangia matokeo hayo na wanajipanga vyema katika michezo ijayo waweze kufanya vizuri.

Naye kocha wa Polisi Tanzanaia, Malale Hamsini amesema kuwa kilichofanya timu yake ishinde waliangalia mkanda na kuisoma vyema Biashara na kabla ya mchezo wa leo pamoja na juhudi za wachezaji wake kujituma uwanjani vimechangia ushindi katika mchezo huo.

Mashabiki wakiburudika uwanjani. (Picha na Fresha Kinasa).

Katika mchezo huo, Biashara United Mara waliwatoa wachezaji wake katika kipindi cha pili akiwemo, Deogratias Judika, Ali Kombo na Lameck Chamukaga na kuwaingiza wachezaji wake Jerome Lambele, Joseph Kimwaga na Gyrishon Samwely.

Kwa upande wa Polisi Tanzania waliwaingiza wachezaji Matheo Anthony na Andrew Chamungu baada ya kuwatoa Erick Msagati na Jimy Shoji wote wakitoka katika kipindi cha pili cha mchezo huo.