Na Suleiman Abeid,Times Majira Online, Shinyanga
JESHI la Polisi Mkoani Shinyanga limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa tisa wanaohisiwa kuhusika na tukio la ujambazi katika kambi ya wachina wanaojenga mradi wa ujenzi wa reli ya mwendokasi (SGR) na kupora vitu mbalimbali ikiwemo bunduki na fedha mbalimbali za kigeni.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Janeth Magomi amesema watuhumiwa hao wamekamatwa kufuatia opresheni maalumu iliyofanyika kwa wiki mbili ya kuwasaka wahalifu na watu waliohusika kwenye tukio la kuvamia kambi hiyo ya wachina huko katika eneo la Old Shinyanga Manispaa ya Shinyanga.
Kamanda Magomi amesema katika opresheni hiyo wamefanikiwa kukamata silaha moja ambayo ni bunduki aina ya Shortgun Pumb Action iliyoporwa kwenye tukio la ujambazi kwenye Kambi ya wachina wanaojenga mradi wa reli ya mwendokasi iliyopo eneo la Old Shinyanga.
Pia wamewakamata watuhumiwa tisa wanaotuhumiwa kuhusika na tukio hilo la kuvamia kambi hiyo ambapo amefafanua kuwa watuhunmiwa kabla ya uporaji walimvamia mmoja wa walinzi aliyekuwa na silaha wakamfunga kamba walipora baadhi ya vitu ikiwemo fedha za kitanzania na za kigeni na kuondoka na silaha.
“Walinzi wa kambi hiyo ndiyo waliokuwa na silaha hii, watuhumiwa hawa walipovamia eneo hilo walimvamia mlinzi aliyekuwa nayo na kumfunga kamba kisha wakaichukua na kuondoka nayo na waliitelekeza kwenye moja ya mashamba ambako iliokotwa ikiwa pamoja na rundo la vitambulisho mbalimbali,”
“Pia katika Opresheni hii tumefanikiwa kukamata lita 910 za mafuta aina ya dizeli yanayotumika kwenye mradi wa ujenzi wa reli ya mwendokasi (SGR), pikipiki nane ambazo zilikuwa zikitumika katika usafirishaji wa mafuta ya wizi, vifaa mbalimbali vilivyokuwa vinatumika katika kuhujumu mradi wa SGR ikiwemo madumu na mipira ya kunyonyea mafuta,” ameeleza Kamanda Magomi.
Amesema katika msako huo pia wamekamata fedha za nchi mbalimbali ikiwemo Naira 16,000 za Nigeria, Dola 100,500 za Vietnam, Yuan 20 za kichina, Dinar 1.5 za Kuwait na Reale 900 za Cambodia zinazohisiwa kuporwa kwenye tukio la uvamizi wa kambi ya ujenzi wa reli ya mwendokasi.
“Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga linatoa wito kwa wananchi hususan vijana, kuacha tabia ya kujihusisha na vitendo vya uhalifu na pia kuacha kufanya hujuma dhidi ya mradi wa reli ya mwendokasi wa SGR kwani Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuwatumikia wananchi wake kwa kuwajengea miundombinu madhubuti hivyo iungwe mkono,” ameeleza.
More Stories
Maghorofa Kariakoo mikononi mwa Tume
ITA chatakiwa kutoa mafunzo ya viwango vya juu na kasi ya maendeleo ya Kisayansi
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi