January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi Rukwa waanza kuwasaka waliomuua bodaboda

Na Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Sumbawanga

JESHI la Polisi mkoani Rukwa linawasaka watu wasiojulikana waliomuua kwa kumkata mapanga muendesha bodaboda aliyefahamika kwa jina la Cassian Laiti(36) nakisha kuiba pikipiki aliyokua anaendesha.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Shadrack Masija aliwaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo lilitokea Februari 24, majira ya saa 5:30 katika mtaa wa Familia Takatifu kata ya Kizwite Manispaa ya Sumbawanga.

Alisema kuwa kabla ya mauaji hayo watuhumiwa hao walikodi pikipiki ya Marehemu na kupanda mshikaki wakimtaka awapeleke nje ya mji kwani walimshawishi kwa kumlipa fedha nyingi naye akakubali asijue kama ulikua ni mtego.

“walipokuwa wakielekea huko, walifika katika mtaa wa Familia Takatifu ndipo walipo mfanyia tukio hilo la kumkata mapanga Kisha kuuacha mwili wake barabarani na kuondoka na pikipiki aina ya Kinglion yenye namba za usajiri MC 173 DEL na Kisha kutokomea nayo kusiko julikana” alisema

Alisema kuwa asubuhi wakazi wa mtaa huo waliuona mwili wa marehemu na kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa mtaa naye akawaita Polisi ambapo walifika eneo la tukio na kuuchukua mwili wa marehemu Kisha kuwakabidhi ndugu zake kwaajili ya maziko.

Hata hivyo kamanda Masija alitoa wito kwa waendesha boda boda kuchukua tahadhari pindi wanapofanya kazi hiyo nyakati za usiku pia wasiwe wanabeba abiria mshikaki kwa ni hatari kwa usalama wao na abiria.

Alisema kuwa Polisi wanaendelea na upelelezi wa tukio hilo ili kuwabaini watuhumiwa wa mauaji hayo na watakapo kamatwa watafikishwa mahakamani ili Sheria ifuate mkondo wake.