November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, ACP Martin Otieno. (Picha ya Azam Tv)

Polisi mkoani Kigoma waua watuhumiwa wa ujambazi 7

Na Mwajabu Kigaza, Kigoma

JESHI la Polisi mkoani Kigoma limethibitisha kuwaua watu saba wanaosadikiwa kuwa majambazi katika eneo la Kumwambu wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma. Watu hao wanatuhumiwa kutaka kufanya uvamizi katika kambi ya kampuni ya ujenzi ya Sino Hydro ambayo inajenga barabara ya Kabingo hadi Mnyovu mkoani humo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma ACP, Martin Otieno aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa tukio hilo lilitokea saa tano usiku wa Aprili 16, mwaka baada ya Polisi kupata taarifa za kuwepo watu wenye njama za kuvamia kambi hiyo ya ujenzi wa barabara.

“Kulikuwa na kundi la watu 12ambao walikuwa wakielekea katika eneo la kampuni hiyo na walipogundua kuwa wanafuatiliwa na askari polisi walianza kurusha risasi na wengine kukimbia,” alisema Kamanda Otieno.

Kamanda Otieno alisema mapambano ya kurushiana risasi yaliyodumu tarkibani dakika 25 na kufanikiwa kuwaua watu watatu eneo la tukio, huku wengine watano wakifariki dunia wakati wakiwa njiani kupelekwa katika Kituo cha Afya Kibondo.

Aidha alisema katika tukio hilo walikata silaha mbalimbali za kivita ikiwemo bunduki zilizotengenezwa kienyeji ambazo zina uwezo wa kutumia risasi za bunduki aina ya SMG. Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za watu wanaosadkiwa ni wahalifu.

Katika hatua nyingine Mkoa wa Kigoma umepokea vifaa kwa ajili ya mawasiliano katika kukabiliana na majanga mbalimbali ya magonjwa pamoja na kutoa elimu ya afya. Vifaa hivyo vimetolewa na shirika la kudhibiti magonjwa la Marekani kupitia Shirika la MDH.

Mkuu wa Mkoa Kigoma Brigedia jeneral mstaafu, Emmanueli Maganga alisema hadi sasa mkoani Kigoma kuna watu 119 ambao wapo karantini.

Idara ya Afya ya Mkoa wa Kigoma imeeleza kuwa huenda ikalazimika kufunga baadhi ya vituo vya afya ikiwa idadi ya watu walio karantini itaongezeka na kuzidi kusistiza kuwa elimu inayotolewa  ya kujikinga na Corona izingatiwe ipasavyo.