April 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi Mbeya yajivunia miaka minne ya mafanikio

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya limesema katika kipindi cha miaka minne,wamefanikiwa kupunguza uhalifu kwa asilimia 3, kutokana na mipango mikakati ya kutumia utaratibu wa kiterejensia .

Hayo yamesemwa April 4,2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi wa jeshi hilo mkoani hapa kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Kuzaga amesema kuwa kwa kipindi cha miaka minne uhalifu umepungua kutokana na ongozeko la rasilimali watu,vitendea kazi pamoja na matumizi mazuri ya ya falsafa ya polisi jamii na ulinzi shirikishi.

“Mafanikio haya yamewajengea uwezo wananchi,kuwabaini wahalifu na utoaji wa taarifa za viashiria vya uhalifu katika maeneo yao,kama Jeshi la Polisi ni hatua kubwa kwetu, tunajivunia,”amesema Kuzaga.

Amesema kuwa mafanikio hayo yamefanya utendaji kazi wa jeshi hilo kuwa mkubwa ikiwa ni pamoja na kuongeza ari kwa polisi ya kufanya kazi.

Pia amesema,katika kipindi hicho wamefanikiwa kuongeza Askari wapya 351 baada ya kumaliza mafunzo ya kijeshi katika Shule ya Polisi Tanzania – Moshi [TPS] zamani CCP na jumla ya Maofisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali 1,162 walipandishwa vyeo katika ngazi mbalimbali.

Sanjari na hayo amesema kuwa jumla ya silaha 40 zisizokuwa na kibali zilikamatwa kati ya hizo gobole 29, S/gun 29, riffle 3 na bastola 2 na risasi 12 za shot gun, goroli 658 na kopo 9 zenye baruti huku tuhumiwa 42 walikamatwa.

Aidha amesema nyara za Serikali zenye thamani ya zaidi ya bilioni 1.6,zilikamatwa na watuhumiwa 33 kukamatwa kati yao wanaume 29 wanawake 4.Pia Wahamiaji haramu 174 walimamatwa kutoka kati yao kutoka nchini Ethiopia 97, Malawi 47, Somalia 19, Burundi 6 na Rwanda 5.

Vilevile amesema kuwa madini ya dhahabu yenye thamani ya ya zaidi ya bilioni 1.8, yaliyokuwa yametoroshwa yalikamatwa na watuhumiwa tisa walikamatwa.

Hata hivyo amesema,wamefanikiwa kupunguza ajali za barabarani kwa asilimia 2.8 ,imechangiwa na kupatiwa vitendea kazi vya kisasa ikiwemo magari mapya kwa ajili ya kufanya doria za barabara kuu (high way patrol) na kipima kasi mwendo (speed rader)

Amesema kuwa pia vifaa vya kupimia ulevi kwa madereva na kuendelea kujiimarisha katika matumizi ya mifumo ya kidigitali ya usalama barabarani ikiwemo matumizi ya mashine ya POS,VTS, TIRA MIS, RAMIS, CMIS, IRTIS na TMS kwa ajili ya kuzuia na kudhibiti makosa ya usalama barabarani na kupelekea kupungua kwa ajali za barabarani.