March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi Mbeya kusaka waliohusika mauaji mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

JESHI la Polisi Mkoani Mbeya linaendelea na uchunguzi wa tukio la mauaji ya aliyekuwa Mwanachuo wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Mzumbe ndaki ya Mbeya kitivo cha sheria aitwaye Shayrose Michael Mabula (21) .

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga  amesema awali mnamo tarehe 14 Septemba, 2025 Baba mzazi wa marehemu aitwaye Dkt.Michael Mabula alifika katika kituo kikuu cha Polisi Mbeya na kutoa taarifa ya kupotea kwa binti yake aitwaye Shairose Mabula ambapo jalada la uchunguzi lilifunguliwa na kuanza ufuatiliaji ili kumpata.

Kamanda Benjamin Kuzaga wa Polisi Mbeya anasema mnamo  Septemba,  16 2025 saa 5 usiku huko katika Kata ya Isyesye Jijini Mbeya ilipokelewa taarifa ya ajali ya moto ambapo Askari walifika eneo la tukio na kukuta kibanda kinateketea kwa moto.

Amesema baada ya uchunguzi ilibainika kuna mwili wa mtu mmoja jinsia ya kike unaungua ambaye kwa wakati huo hakuweza kutambulika na mwili wa marehemu ulichukuliwa na kuhifadhiwa Hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya.

Kuzaga amesema kuwa  baada ya uchunguzi wa kitabibu na kuhusisha ndugu ilibainika kuwa mwili huo ni wa Shairose Mabula aliyekuwa anatafutwa baada ya kuripotiwa kupotea.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na uchunguzi wa kina ikiwemo uchunguzi wa kisayansi ili kubaini na kutambua mwili wa marehemu na kuwakamata waliohusika na mauaji ya binti huyo.

Pia jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa azitoe ili mkondo wa sheria kufuatwa ambapo pia Polisi mkoani Mbeya inaendelea kutoa rai kwa jamii kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo mauaji.