December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi: Maandamano ya kudai Tume Huru marufuku

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

KAMANDA wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ametoa onyo kali kwa wananchi waliopanga kufanya maandamano leo yakihamasisha uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi nchini.

RPC Mambosasa amefikia uamuzi huo baada ya kuwepo taarifa kwenye mitandao ya kijamii zikieleza kuwa wananchi hao watafanya maandamano leo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mambosasa amesema Tume Huru ya Uchaguzi haipo mkoani Dar es Salaam na kwa hiyo watu hao hawatakiwi kulipima Jeshi la Polisi.

“Nitoe onyo Tume Huru inayodaiwa haipo Dar es Salaam, lakini Tume ya Uchaguzi pia haipo Dar es Salaam Makao Makuu yake yapo Dodoma, kitendo cha watu kuja kufanya maandamano Dar es Salaam ni uchokozi wa kupimana,” amesema.

Amesema kupimana huko si kwa namna nzuri kwani matokeo yake hayatakuwa mazuri kwa atakayejaribu kufanya maandamao hayo. “Niwaonye wote wanaohamasishana waishie huko huko kwenye mitandao ya kijamii, wasijaribu kutoka kwenye mitandao wakaenda kwenye ardhi hii ambayo tumekabidhiwa kuhakikisha watu wetu wanaendelea kuwa salama hawataenda zaidi ya hatua tano,” amesema.

Ameongeza kuwa matokeo ya kukaidi kutokufanya maandamano ni kilio, kwani ni kinyume na sheria. Amesema hajapata maombi yoyote kuhusiana na kuwepo kwa maandamano hayo katika mikoa yote mitatu ya Kipolisi ya Ilala, Kinondoni na Temeke.

Amesema Tanzania imeingia kwenye uchumi wa kati hivyo ni muhimu kila mwananchi akachangamkia fursa ya kutafuta kipato kilicho halali, kwani atakayejaribu kuwapima uwezo wao kwa kuleta fujo mkoani mwake, wamejipanga kuwathibiti.

“Tumejipanga si tu katika maandamano hayo, lakini tumejipanga kuhakikisha kipindi chote cha mchakato kuelekea uchaguzi mkuu, mchakato wa upigaji kura, uhesabuji kura na lile shangilio la aliyeshinda kwa usawa,”amesema.

“Niwaombe Watanzania waendelee kuheshimu sheria za nchi bila kushurutishwa, anayetaka kushurutishwa tupo tutamuwezesha kutii sheria, lakini anayetii sheria kwa hiari ataendelea kuwa salama na kuheshimika,” amesema.