December 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polepole amkabidhi Shaka mikoba ya uenezi CCM

Na Penina Malundo, Timesmajira,Online

KATIBU wa Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi, Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka akabidhiwa rasmi ofisi ya Idara ya Itikadi na Uenezi leo na aliyekuwa Katibu wa Halmsahauri kuu ya CCM katika idara hiyo, Humphrey Polepole, Ofisi ndogo ya Makao Makuu ya CCM lumumba.

Akizungumza leo baada ya makabidhiano hayo ya Ofisi,Katibu huyo mpya Shaka Hamdu Shaka amesema Chama hicho kimempongeza Katibu Mkuu wa CCM,Daniel Chongolo kwa kuanza kutoa mwelekeo na dira ya majukumu ya sekretarieti ya nec kwa muktadha kuisimamia na kufuatilia utendaji wa Serikali utakoleta tija na manufaa kwa umma.

Amesema sekreterieti ya nec haitakuwa tayari kuona watanzania wakihangaika ,kutahabika na kukosa haki za msingi, au kufanyiwa dhuruma na udhalilishaji wa aina yoyote.

Shaka amesema ni kawaida yanapotokea mabadiliko wahusika kukabidhiana kazi za kiofisi na kuongeza kusema kama kazi ya utendaji za ccm , katibu mkuu chongolo ni kama upele ulimopata mkunaji kutoka na upeo alionao kisiasa na kiutendaji

Amesema atakuwa tayari kutoa kila alichonacho kusaidiana na wenzake lakini pia atakuwa tayari kupokea na kujifunza kutoka kwa wenzake akichukua na kupokea mawazo, ushauri, miongozo na kuwa mjasiri wa kusimamia changamoto chini ya shabaha na malengo ya CCM

Amezitaka taasisi za umma na za kiserikali kila moja kutimiza wajibu wake kwa kutumikia na kufuata miongozi ya kisera na malengo ya kimkakati yilioainishwa kwenye ilani ya uchaguzi ya ccm ya mwaka 2015/2020.

“Wote ni mashahidi Rais Samia Suluhu Hassan amechukua jitihada za wazi za kujenga mahusiano yanayochochea msukumo wa biashara na uwekezaji,ameondoa vizuizi vya kibiashara kwa manufaa ya wote na amewahimiza wafanyabiashara na wananchi kulipa kodi,kodi isiwe bughudha na kizuizi bali kila mmoja alipe kwa wakati na hiari “Amesema shaka

Amesema Rais Samia ana nia ya dhati na kweli amedhamiria kujenga nchi huku akitaka iende kwa mwendo wa haraka ndio maana ameanza kufungua milango iliotaka kujifunga akifuata nyayo za watangulizi wake ambao wote walipikwa, kuandaliwa na kupewa dhamana uongozi na CCM.