Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Monduli
Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda,amewahimiza wananchi kumuenzi Hayati Edward Lowassa aliyekuwa Waziri Mkuu Msaafu kwa kutenda na kuyaendeleza matendo mema aliyotafanya kipindi cha uhai wake.
Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda ametoa kauli hiyo Februari 16,2024 wakati akiongoza mamia ya waombolezaji kuaga mwili wa Hayati Edward Lowassa nyumbani kwake katika Kijiji cha Ngarash wilayani Monduli mkoani Arusha ambapo Lowassa atazikwa kesho Februari 17, 2024 katika ibada itakayohudhuriwa pia na Rais Samia Suluhu Hassan.
Pinda ameeleza kuwa kila mmoja kutumia nafasi hii ya kumuenzi aliyekuwa Waziri Mkuu huyo kwa kutenda yale mema aliyofanya kipindi cha uhai wake.
Amesema, yeye amejifunza mengi kupitia Hayati Lowassa, kipindi cha uhai wake alipokuwa akifanya nae kazi, huku akidai kuwa hata alivyo leo ni kutokana na mchango wake.
” Wakati akiwa Waziri Mkuu mimi nilipata bahati ya kufanya nae kazi, nilikuwa chini yake hivyo nilijifunza mengi sana kwani Hayati Edward Lowassa alikuwa ni mtu asiyependa kushindwa alikuwa ananiambia hili lazima tufanye na kweli linafanyika,ukimwambia pole na kazi anasema tupongezane badala ya kupeana pole kwani tumefanikisha”, ameeleza Pinda.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, amesema Serikali itaendelea kutambua mchango wa aliyekuwa Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Ngoyai Lowassa katika kipindi cha utumishi wake.
Pia, amesema ni vyema kujenga tabia ya kuwaombea viongozi kipindi cha utumishi wao, ili waweze kutimiza majukumu yao kwa ufasaha.
” Tunatoa pole kwa familia nzima kwa kweli tumepoteza kiongozi mahiri na aliyekuwa mtu wa watu kama mnavyoshuhudia kwa kila mmoja jinsi anavyomuelezea, sisi kama Serikali tutaendelea kutambua mchango wake katika kipindi chote alichohudumu serikalini na hata kwenye chama cha CCM,”amesema Jenista.
Naye Kiongozi wa kimila wa kabila la Wamasai, Isack Lekisongo Meijo, amesema wanaipongeza Serikali kwa kutoa fursa kwa kila mtu kuweza kushiriki katika shughuli za kumuaga Lowassa, huku akieleza kuwa mila za jamii ya kimasai zitatumika katika mazishi yake.
More Stories
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM