


Na Joyce Kasiki,Dodoma
JAMII imetakiwa kufanya upandaji wa miti kuwa sehemu ya maisha ya kila siku badala ya kusubiri matukio maalumu ya viongozi, ikiwa ni jitihada za kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutunza na kulinda mazingira nchini na kukabiliana na madiliko ya tabianchi.
Wito huo umetolewa leo jijini Dodoma na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, wakati wa zoezi la upandaji wa miti 1,000 lililofanyika katika eneo la Njedengwa, mkoani Dodoma. Zoezi hilo lilihusisha Taasisi ya Habari Conservation, wakazi wa eneo hilo pamoja na wanafunzi kutoka shule mbalimbali.
Pinda amesema jamii haipaswi kusubiri matukio makubwa kama siku za kuzaliwa za viongozi ndipo ianze kampeni za upandaji miti, bali ihakikishe zoezi hilo linafanyika mara kwa mara kama utamaduni wa kudumu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Wananchi kuanzia ngazi ya kata hadi taifa kwa ujumla, tunapaswa kuwa na utaratibu wa kupanda miti bila kusubiri msukumo kutoka kwa viongozi. Mfano siku ya kuzaliwa ya Rais isiwe ndiyo kigezo pekee, bali tujitume wenyewe kila wakati,” alisema Pinda.
Aliongeza kuwa kila Mtanzania anatakiwa kutambua umuhimu wa mazingira kwa kupanda miti ya aina mbalimbali ikiwemo ya kivuli na ya matunda, ili kusaidia kuboresha hali ya hewa na ustawi wa maisha ya jamii.
Aidha, Pinda alimshauri Mkuu wa Mkoa wa Dodoma pamoja na Taasisi ya Habari Conservation kutumia vikundi vya vijana, hususan wanaojihusisha na mazoezi ya asubuhi kama kukimbia (mchamchaka), kuwahamasisha kushiriki kampeni za upandaji miti. Amesema vijana wana nguvu na ushawishi mkubwa katika jamii na wanaweza kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika uhifadhi wa mazingira.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kudhibiti Manunuzi ya Umma (PPRA), Dennis Simba, aliipongeza Taasisi ya Habari Conservation kwa kujikita katika masuala ya mazingira kwa lengo la kuisaidia serikali kutunza mazingira.
Amesema PPRA imeingia makubaliano ya udhamini wa mwaka mmoja na taasisi hiyo baada ya kujiunga na mfumo wa NesT unaotumika na serikali katika kufanya manunuzi.
Simba aliongeza kuwa PPRA itaendelea kushirikiana na taasisi hiyo kuhakikisha miti iliyopandwa katika eneo la Njedengwa na maeneo mengine inatunzwa ipasavyo, huku akiomba taasisi nyingine kujiunga na mfumo wa NesT ili kuboresha uwazi katika manunuzi na kushiriki katika shughuli za kijamii ikiwemo uhifadhi wa mazingira.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alisema mkakati wa mkoa ni kuhakikisha maeneo yote yaliyoainishwa yanapandwa miti ili kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Amesema katika msimu uliopita mkoa ulifanikiwa kupanda miti 40,000 na matarajio ni kuongeza idadi hiyo katika misimu ijayo.
Naye mwakilishi wa Taasisi ya Habari Conservation, Loyce Obongo, amesema taasisi yao imejipanga kushirikiana na serikali na wadau wengine katika kutekeleza miradi ya upandaji na utunzaji wa miti, pamoja na kuhamasisha jamii kuchukua wajibu wao katika kulinda mazingira.

More Stories
Kihongosi amtaka mkandarasi kuwalipa vibarua stahiki zao
DC Mbozi afuturisha wananchi, asisitiza mshikamano na Umoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Nina imani mubna utendaji kazi wa ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria