Na George Mwigulu, Timesmajira Online,Katavi
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amewasihi wananchi kuugana na Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Kayanza Peter Pinda anayetarajiwa Oktoba 29 mwaka huu kwenda kutalii katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi ikiwa ni sehemu ya maonesho ya wiki ya Mwanakatavi.
Amebainisha hayo Mkuu wa Mkoa huyo katika viwanja vya CCM Azimio Manispaa ya Mpanda ambapo ameeleza maonesho hayo yamelenga pia kutangaza na kukuza utalii wa ndani kupitia kuwajengea wananchi tabia ya kufahamu nchi yao na vivutio vyake utakao chochea kuongeza mapato sekta ya utalii.
Mrindoko amesema kuwa Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda ambaye ni Mwanakatavi mashuhuli uwepo wake ni muhimu kwa kuwa kielelezo bora zaidi kwa wananchi utakao jenga uzalendo wa watu kupenda nchi yao na kutumia fursa ya kutalii.
Maonesho ya Mwanakatavi yanaunga mkono Royal Tour iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassain ambapo matokeo yake ni kushuhudiwa kwa ongezeko la watalii wengi katika Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini ikiwemo Katavi wamekuwa wakifika kuona vivutio mbalimbali.
Amefafanua kuwa licha ya maonesha ya utalii hufanywa Nyanda za Juu Kusini lakini wameona kuna tija kubwa kuwasogezea kwa karibu wananchi huduma ya kuona wanyama hai katika uwanja huo ili kutoa hamasa ya kwenda kutembelea Hifadhi ya Taifa yenye vivutio vya kila aina.
“Pamoja na hayo tunasafari kwenda Katavi National Park Oktoba 29 mwaka huu niombe kila mmoja asipange kukosa tunakwenda kuona maliasili nzuri ambazo Mwenyezi Mungu ametutunuku Mkoa wa Katavi tutakwenda kuona wanyama wa aina mbalimbali,”amesema.
Amesisitiza kuwa licha ya baadhi ya wanyama kama Simba na Chui wanapatikana kwenye maonesho ya wiki ya Mwanakatavi ni jambo muhimu kwenda katika Hifadhi ya Taifa kujionea makundi makubwa ya viboko ambao wanaishi pamoja tembo wenye maumbo makubwa zaidi kuliko wa maeneo mengine,twiga,mamba,nyati na wengine wengi.
Jackson Faustine,Mkazi wa Mtaa wa Makanyagio amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko kwa kuanzisha Wiki ya Mwanakatavi ambapo imewasaidia kuona wanyamapori ambao hawakuweza kuwaona hapo awali.
“Niwe mkweli naishi hapa Katavi sasa kwa muda wa miaka saba sijawahi kuona simba wala chui naambiwa wanapatikana katika hifadhi ya taifa ya Katavi,kutokana na majukumu ya familia nimeshida kufika huko lakini leo nimewaona,”amesema.
Neema Paschal,Mkazi wa mtaa wa Misukumilo amesema ujio wa Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda utachochea zaidi wananchi kuona umuhimu wa kwenda kutembelea hifadhi ya taifa kwa kuwa amekuwa kiongozi wao kwa muda mrefu na anawafuasi wengi wanaomfuatilia kwa lengo la kujifunza mambo kutoka kwake.
Ameiomba serikali ya Mkoa huo kuendelea zaidi kutoa hamasa kwa wananchi kushiriki na kuchangamkia fursa za utalii hususani kuwavutia zaidi wawekezaji watakao jenga hotel za hadhi kubwa ambazo zitatumiwa na watalii.
More Stories
Maofisa Watendaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi
Muhoji Sekondari kumaliza changamoto ya umbali kwa wanafunzi Musoma vijijini
Tanzania mwenyeji mkutano wa nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika