Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
KATIKA kuunga mkono dhamira ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda ya kuendeleza michezo yote nchini kwa vitendo, Shule ya kimataifa ya Monti International School imetangaza kuandaa kambi maalum ya kuogelea ya siku 10 itakayoongozwa na kocha maarufu kutoka Marekani, Austin Pillado.
Kambi hiyo ya kiwango cha juu inatarajiwa kufanyika kuanzia Mei 5 hadi Mei 14, 2026 katika kampasi ya Mikocheni, jijini Dar es Salaam.
Kocha Pillado, ambaye ni Naibu Kocha Mkuu wa timu ya wanawake ya kuogelea kutoka Chuo Washington State, pia alikuwa sehemu ya benchi la ufundi lililoshinda ubingwa wa mashindano ya juu kabisa ya michezo ya vyuo vikuu nchini Marekani, yanayoandaliwa na National Collegiate Athletic Association (NCAA) mwaka 2024 akiwa na Arizona State University.
Akiwa na uzoefu wa kufanya kazi na mabingwa wa Olimpiki na washikiliaji wa rekodi za dunia, ujio wake unatajwa kuwa hatua muhimu kwa maendeleo ya michezo ya vijana nchini.Akizungumza kuhusu tukio hilo, Mkurugenzi mkuu na Mwanzilishi wa shule hiyo, Fatma Fernandes alisema lengo kuu ni kuinua viwango vya vipaji vya ndani kufikia hadhi ya kimataifa.

“Tunataka kuziba pengo kati ya vipaji vya ndani na viwango vya kimataifa. Kwa kuwaleta makocha wa kiwango cha juu kama Austin, tunawezesha vijana wetu kupata mafunzo na uchambuzi wa kitaalamu sawa na wanariadha bora duniani,” alisema Fernandes.Kambi hiyo itakuwa ya kwanza katika ukanda huu kutumia teknolojia ya kamera za chini ya maji (underwater cameras) inayotoa mrejesho wa papo kwa papo kuhusu mbinu za waogeleaji.
Mbali na mazoezi ya kimwili, washiriki watapata mafunzo ya ziada kuhusu mikakati ya mashindano, lishe bora na mbinu ya “Fifth Stroke” inayohusisha mbinu za uogejeleaji ambazo ni muhimu katika ushindani wa kisasa.

Kwa mujibu wa waandaaji, programu hiyo imeundwa kwa kuzingatia mitaala ya vyuo vikuu vya Marekani vinavyoshiriki mashindano ya NCAA, ikilenga kuimarisha stadi za mbinu nne kuu za kuogelea pamoja na kuendeleza uwezo wa uvumilivu na kasi.
Uongozi wa Monti umeeleza kuwa uwekezaji katika miundombinu ya michezo, ikiwemo bwawa la kisasa la mita 25 la kiwango cha Olimpiki, una lengo la kunufaisha si wanafunzi wa shule hiyo pekee bali pia jamii pana ya Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla.

Kambi hiyo pia inatarajiwa kuvutia washiriki kutoka nchi jirani za Afrika Mashariki, huku nafasi zikitajwa kuwa chache ili kuruhusu ufuatiliaji wa karibu wa maendeleo ya kila mshiriki.Hatua hiyo inaonekana kuwa mchango mkubwa katika kuiweka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa ya mchezo wa kuogelea, huku ikienda sambamba na malengo ya Baraza la Michezo nchini (BMT) ya kuendeleza, kuratibu, na kudhibiti michezo.

More Stories
DCEA yapokea vifaa vya kisasa kutoka UNODC
Pre-Betika Tulia Marathon kuwainua kiuchumi vijana Mbeya
Watumishi NIRC washerehekea mwaka 2026,waaswa kuimarisha mshikamo,uwajibikaji