January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Pata undani wa kilichotokea Kijijini Mbezi Beach B (PICHANI)

Na Waandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam

MIAKA 30 ya kuvuta bangi, kutumia dawa za kulevya, unywaji wa pombe haramu ya gongo na ngono ya nipe nikupe imehitimishwa alfajiri ya kuamkia Desemba 9, mwaka huu baada ya Serikali kubomoa mabanda zilipokuwa zikiishi kaya kati ya 30 hadi 40 zilizogeuza eneo la Kijiji, Kata ya Kawa Mtaa wa Mbezi Beach B, wilayani Kinondoni ngome ya uhalifu.

Iliyokuwa bar ya kiongozi mmoja wa CCM aliyekuwa anatetea uhalifu katika eneo la Kijijini ilikumbwa na bomoabomoa pembezoni mwa barabara mbele ya Mgahawa wa Juliana, Mbezi Beach B, Kata ya Kawe, Kinondoni, Dar es Salaam

Eneo la Kijijini lililopo Mtaa wa Mbezi Beach B, ni moja ya eneo ambalo wakazi wake walijenga makazi katika hifadhi ya barabara, wakifanya biashara ya haramu.

Mabanda hayo yalibomolewa Jumamosi alfajiri ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, baada ya siku 14 alizowapa wakazi hao kuhama kwa hiari kumalizika.

Ubomoaji wa mabanda hayo ulianza Jumamosi alfajiri bila kujali mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mtaa wa Mbeazi Beach.

Wakati zoezi hilo likiendelea wakazi wa eneo hilo walisikika wakilia, huku kukiwa kwenye hekaheka ya kujaribu kuokoa mali zao bila kujali mvua kubwa iliyokuwa ikiendelea kunyesha.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo ambaye jina lake halikupatikana, alisikika akilaumu baadhi ya viongozi wa chama wa mtaa huo, akisema waliwataka kuendelea kuishi eneo hilo, wakati muafaka ukitafutwa ngazi za juu.

Wafanyakazi wa Halmashauri wakiendelea kufanya usafi baada ya bomoabomoa pembezoni mwa barabara mbele Mbezi Beach B, Kata ya Kawe, Kinondoni, Dar es Salaam

“Wenyewe wanaitaka barabara yao, bora tungebomoa wenyewe maana tuliambiwa, lakini ubishi umetufikisha hapa. Tumeponzwa na hawa viongozi uchwara, waliotuambia hatutaondoka sababu wao ndio wenye duka (CCM),” alisema na kuongeza;

“Walituambia Mkuu wa Wilaya ni msimamizi tu wa duka, sasa leo msimamizi wa duka ndio kasimamia duka, sasa hapo nani zaidi?”

TimesMajira Online hili ilishuhudia zoezi la ubomoaji likiendelea, huku kukiwa na hekaheka za kuokoa vitu mbalimbali. Miongoni mwa waliokuwa kwenye hekaheka za kuhamisha mali zao ni pamoja na mwanamke ambaye alijipatia umaarufu kwa kusokota bangi.

Mwanamke huyo alisikika akiangua kilio huku akisema atakuwa mgeni wa nani huko anakokwenda.

Ubomoaji wa mabanda hayo ulisimamiwa na wafanyakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ambao walikuwa wakikusanya mabati na mbao na kuzipakia kwenye lori lenye namba za usajili SM12739.

Nao askari wa Jeshi la Polisi waliokuwa wakisimamia zoezi hilo walipoulizwa kuhusu mwenendo wa zoezi hilo, walisema hapakuwa na upinzani wowote, wala kizuizi chochote na kwamba wakazi hao walitoa ushirikiano kwa kukusanya wenyewe vitu vyao.

Mmoja wa waathirika wa bomoabomoa Mbezi Beach B, Kata ya Kawe, Kinondoni, Dar es Salaam akitafakari maisha baada ya tukio hilo

“Hakuna vurugu yoyote, hakuna upinzani wala aliyekaidi, sisi kama Polisi tuko hapa kuhakikisha kuna amani na zoezi hili linakamilika bila ubishi wala kikwazo chochote,” alisema mmoja wa askari ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa madai kuwa sio msemaji wa jeshi hilo.

Baadhi ya wakazi waliongea na mwandishi wa TimesMajira Online kwa kumshukuru Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dares Salaam kuhakikisha wakazi wa Kijijini wanaondoka

Mkazi wa Mbezi Beach (Block H Maliasili) Mhandisi Jesse Kahwa alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kwa jitihada zake za dhati kuondoa kero hiyo kwa kusambaratisha makazi hatarishi yalioshindikana katika moja ya barabara mtaa wa Kijijini uliodumu kwa kipindi kirefu.

“Pokea Pongezi na shukrani za dhati kutoka Kamati ya Ulinzi ya Mtaa, Wazee Wastaafu na majirani wote wapenda amani na maendeleo katika mitaa yetu, pamoja na pongezi zangu binafsi,” alisema na kuongeza Mhandisi Kahwa;

“Tunakuomba hao viongozi wapotoshaji wamulikwe na kuchukuliwa hatua kwa kuchochea ukaidi katika jamii!”

Naye Wakili Msomi Ibrahim Bendera, ambaye ni MwenyeKiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama katika mtaa huo, alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kwa kusikiliza na kusimamia sheria ambayo imewafanya wanachi hao kwa sasa kuwa na amani katika eneo hilo.

Mmoja wa wakazi wa eneo la Kijijini akiendelea kukusanya baadhi ya vitu baada ya bomoabomoa Mbezi Beach B, Kata ya Kawe, Kinondoni, Dar es Salaam

“Kilichopo sasa ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa kuhakikisha kila mwenye nyumba katika eneo la barabara linalopakana na nyumba yake ni pasafi, usiku pana taa inayotoa mwanga wa kutosha.

Naye Mkazi wa Mtaa huo wa Mbezi Beach Block H, Aban Mtui alisema yupo katika mtaa tangu mwaka 1999, tatizo la uvutaji bangi na dawa za kulevya katika Mtaa wa Kijijini ni la siku nyingi.

Matokeo ya kusambaratishwa kwa makazi ya uhalifu baada ya bomoabomoa Mbezi Beach B, Kata ya Kawe, Kinondoni, Dar es Salaam