November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Pareso achangia saruji mifuko 100, ujenzi jengo la mama na mtoto

Na Sophia Fundi, Timesmajira Online,Karatu

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha Cesilia Pareso ametoa mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto zahanati ya kijiji cha Upper Kitete.

Mbunge Cesilia alitoa saruji hiyo Julai 17,2024 baada ya wananchi wa kijiji hicho kueleza changamoto ya ukosefu wa jengo hilo katika zahanati yao ya Upper Kitete katika mkutano wake ambapo walieleza adha wanayopata wajawazito wakati wa kujifungua.

Akieleza changamoto ya ukosefu wa jengo hilo Anna John mkazi wa kijiji hicho amesema wamekuwa wakiteseka kufuata huduma ya uzazi umbali mrefu jambo ambapo ni hatari na kuweza kusababisha vifo kwa wajawazito na watoto hivyo ameomba Mbunge huyo kusaidia katatua changamoto hiyo.

Katika ziara yake Mbunge huyo amepokea kero mbalimbali za wananchi ikiwemo ya wanyama wanaovamia kwenye makazi ya watu na kuleta uharibifu mkubwa wa mazao.

“Tunaomba utusaidie huko bungeni suala la wanyama kuvamia makazi ya watu na kuharibu mazao yao,kwa nini kila siku tunalia na wanyama hao bila serikali kutusaidia,tunakutuma sisi wananchi tulioko pembezoni mwa msitu wa Ngorongoro utuwakilishe tupate suluhisho la kudumu la wanyama hao,”amesema Josphat Burra.

Ambapo ameiomba serikali kuja na mkakati wa kudumu wa kudhibiti wanyama hatarishi wanaovamia kwenye mashamba ya wananchi na kuharibu mazao yao na kusababisha vifo kwa baadhi ya maeneo.

Mbunge huyo Yuko kwenye ziara ya kusikiliza kero za wananchi katika wilaya ya Karatu ambapo pia amezungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Slahhamo na Upper Kitete ambapo aliwasihi wanafunzi kusoma kwa kuweka nia na kufikia ndoto zao za baadae.