Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
KIONGOZI wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, amefariki dunia kwa amani siku ya Jumatatu ya Pasaka akiwa na umri wa miaka 88. Baba Mtakatifu alifariki saa 1:35 asubuhi katika makazi yake ya Casa Santa Marta ndani ya mji wa Vatikani.

Taarifa rasmi ya kifo chake ilitolewa na Kardinali Kevin Farrell, Camerlengo wa Chumba cha Kitume, ambaye aliwahutubia waumini kwa huzuni:
“Ndugu wapendwa, kwa huzuni kubwa natangaza kifo cha Baba Mtakatifu Francis… Maisha yake yote yalikuwa ni ya huduma kwa Bwana Yesu na kwa kanisa lake. Alitufundisha kuishi maadili ya injili kwa uaminifu, ujasiri, na upendo wa wote, hasa kwa maskini na waliotengwa. Kwa shukrani kubwa kwa mfano wake kama mfuasi wa kweli wa Yesu Kristo, tunamkabidhi roho ya Papa Francis kwa upendo wa huruma usio na kikomo wa Mungu wa Utatu Mtakatifu.”
Akiwa amezaliwa kama Jorge Mario Bergoglio huko Buenos Aires, Argentina, Papa Francis alikuwa Papa wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini na mwanajumbe wa kwanza wa Shirika la Kijesuiti kuchaguliwa kuwa Papa, mwaka 2013. Kipindi chake cha upapa kilitambulika kwa unyenyekevu, huruma, utunzaji wa mazingira, na kujitoa kwa ajili ya wanyonge.
Afya ya Baba Mtakatifu imekuwa ikizorota katika miaka ya hivi karibuni. Mnamo Februari 2025, alilazwa katika Hospitali ya Agostino Gemelli mjini Roma baada ya kuugua bronchitis kwa siku kadhaa. Baadaye, madaktari waligundua kuwa alikuwa na nimonia pande zote za mapafu. Baada ya siku 38 hospitalini, alirudi Casa Santa Marta kuendelea kupona akiwa nyumbani.
Papa Francis amekuwa akikumbwa na matatizo ya mfumo wa upumuaji tangu ujana wake. Mnamo mwaka 1957, akiwa kijana nchini Argentina, alifanyiwa upasuaji wa kuondoa sehemu ya pafu lililoathirika na maambukizi makali ya njia ya hewa. Katika uzee wake, mara kwa mara alikuwa akiugua magonjwa ya kupumua. Mnamo Novemba 2023, alifuta safari yake kwenda Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kutokana na mafua na uvimbe kwenye mapafu.
Licha ya changamoto za kiafya, aliendelea kutimiza majukumu yake ya kichungaji na kiroho. Mnamo Aprili 2024, mwaka mmoja kabla ya kifo chake, aliidhinisha toleo jipya la kitabu cha liturujia ya mazishi ya mapapa—ambacho sasa kitaongoza misa yake ya mazishi. Toleo hilo jipya la Ordo Exsequiarum Romani Pontificis linalenga kurahisisha ibada, kulingana na ombi la Papa mwenyewe, akisisitiza kwamba mazishi yake yawe ya kiimani zaidi kuliko ya kifalme.
Kwa mujibu wa Askofu Mkuu Diego Ravelli, Mwalimu wa Sherehe za Kipapa, Papa Francis alitaka ibada hiyo ioneshe kuwa:
“Mazishi ya Baba Mtakatifu ni ya mchungaji na mfuasi wa Kristo, si ya mtu mwenye mamlaka ya kidunia.”
Tarehe na utaratibu wa mazishi yake bado haujatangazwa rasmi. Maelfu ya waamini kutoka duniani kote wanatarajiwa kuelekea Vatikani kwa siku zijazo ili kutoa heshima zao za mwisho kwa Papa aliyesimama kama mfano wa unyenyekevu, huruma, na upendo wa kweli.
More Stories
Rais Samia aomboleza kifo cha Papa Francisko
Kanisa la Shincheonji la Yesu nchini Ufaransa lakanusha ripoti ya Le Parisie
Vyombo vya ulinzi na usalama Mbeya,Benki kuu kushirikiana kutatua changamoto za utapeli mtandaoni