December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PAC yaridhishwa na ujenzi wa ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa

Na Mwandishi Wetu Dodoma, Timesmajira Online

MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu, Naghenjwa Kaboyoka, ameeleza kuridhishwa na Maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa unaendelea katika eneo la Kilimani Mkoani Dodoma.

Kaboyoka ameyasema hayo mapema wiki hii, akiwa Jijini Dodoma wakati kamati hiyo ilipofanya ziara yake ya kutembelea mradi huo, ili kukagua maendeleo ya ujenzi na kupata taarifa ya matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya mradi huo.

” Kwakweli mradi unaendelea vizuri sana na tumejionea kuwa umejengwa kwa kiwango na ubora unaotakiwa na tumeona vifaa vya kuendelea ujenzi vipo vya kutosha, lakini pia tumeona thamani ya fedha zilizotumika zinaakisi ukubwa wa kazi iliyofanyika, hivyo tunaamini kazi hii itakamilika kwa viwango sahihi”, amesema Naghenjwa.

Akisoma taarifa ya maendeleo ya ujenzi huo mbele ya kamati, Mshauri Mwelekezi kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi, Mhandisi Denatus Dominick, alisema kuwa, mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 20.4, fedha ambazo zimetumika kujenga jengo la ghorofa sita lenye vyumba vya ofisi 115, kumbi za mikutano saba, maktaba moja, sehemu za maegesho ya magari, uzio, sehemu ya kulia chakula, mfumo wa maji taka nk

” Mpaka sasa mradi huu umetekelezwa kwa takribani asilimia zaidi ya 80 kwa kazi ya jengo Kuu na kazi za inje asilimia 30 kwa kazi za mifumo ya umeme na mitambo na mradi huu umetumika kama sehemu ya mafunzo kwa vijana kutoka vyuo mbalimbali wanapokuja kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo kwani pia umetoa ajira za muda mfupi kwa wazawa, lakini pia mradi huu utakapokamilika utaongeza Pato la nchi, kupitia ukodishwaji wa kumbi zilizopo kwenye jengo hili. Amesema Dominick.

Amemaliza kwa kusisitiza kuwa, mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia ubora na kusema kuwa, watajitahidi kusimamia kwa uwadilifu ili umradi huo uwezw kukamilika kwa wakati.

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ambayo hivi sasa ipo chini ya Jaji Fransis Mutungi, ilianzishwa mwaka 1992, huku moja ya lengo Kuu ikiwa ni uwepo wa ukuaji wa demokrasia ya Vyama Vingi nchini pamoja na usimamizi wa sheria ya Vyama vya Siasa Na 5.

Ambapo hivi sasa Jaji Mutungi akiwa anaendesha mabaraza mbalimbali yanayowahusisha viongozi wa Vyama mbalimbali vya siasa, amekuwa akiunga mkono juhudi za Rais Dkt. SamiaSuluhu Hassan, za matumizi ya R4 kwa ajili ya ustawi wa nchi.