April 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PAC yaipongeza Serikali kujenga maabara ya Uidhinishaji vifaa vya Mawasiliano ya kieletroniki

Na Mwandishi wetu Timesmajira

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeipongeza  Serikali chini ya Uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kujenga maabara ya Uidhinishaji wa vifaa vya Mawasiliano ya kieletroniki(TAL) na kueleza kuwa ni fursa kwa Nchi kunufaika kiuchumi pamoja na kuondoa hofu kwa wananchi juu ya vifaa feki vya kieletroniki vinavyoingia nchini.

Akizugumza mara baada ya kumaliza ziara ya kukagua na kutembelea mradi wa  maabara hiyo, Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka amesema Mradi wa maabara hiyo umetekelezwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),

Kaboyoka amesema kupitia maabara hiyo nchi ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika teknolojia hiyo ambayo inahakikishia wananchi kutokuwa na wasiwasi na vyombo vya kieletroniki vinavyoingia nchini ambavyo vinaweza kuweka Nchi katika hali mbaya.

“Maabara hizi zipo katika hatua kubwa ya  kimataifa nampongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha  zilizotumika kujenga maabara hii ambayo Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi ya 12 Afrika kuwa na maabara ya aina hii”amesema

Aidha ameupongeza Uongozi wa  TCRA kwa kuweza kujifunza namna ya kuendesha maabara hiyo ambayo inaweka nchi ya Tanzania katika hatua kubwa sana ya kimataifa.

“Maabara hii imeweza kutuonesha kwamba huko mitaani watu wamekuwa na wasiwasi kuhusu simu feki au zina  madhara lakini TCRA wametuonesha jinsi ambavyo wanapima na kuona kwamba simu wanazotumia wananchi aziwezi kuwadhuru katika afya zao”amesema

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt.Jabiri Bakari  amesema maabara ya uidhinishaji wa vifaa vya Mawasiliano ya kieletroniki ni maalumu kwa ajili ya upimaji wa vifaa vya Mawasiliano ya kieletroniki ili kuhakikisha vimekidhi viwango husika .

Akitaja Faida za maabara hiyo Dkt.Bakari amesema  imeongeza ufanisi na uwezo wa kuhakiki vifaa vya Mawasiliano ya kieletroniki kama vinaendana na taarifa za vipimo zinazowasilishwa kutoka kwa wategenezaji, pamoja na kuwezesha upimaji wa vifaa ambavyo tayari vipp kwenye soko la Tanzania ili kuhakikisha vinaendelea kukidhi vigezo vya matumizi

Aidha amesema TCRA itaendelea kusimamia uidhinishaji wa vifaa vya Mawasiliano vya kieletroniki ili kuhakikisha vinakidhi vigezo vya matumizi na kuendelea kutoa elimu kwa umma.