March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Othman: Umoja wetu ndio silaha ya kuiondoa CCM

Na Mwandishi Wetu, Micheweni

Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ambaye pia alikuwa mgombea wa urais wa Zanzibar katika uchaguzi uliopita, amewataka wanachama wa chama hicho kuendeleza umoja wao ambao alisema ndio uliopelekea chama hicho kupata ushindi mkubwa.

Othman ametoa wito huo wakati akizungumza na wanachama wa ACT Wazalendo katika ukumbi wa afisi ya Jimbo la Micheweni, Pemba, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kuwashukuru wanachama na wananchi waliowaunga mkono katika uchaguzi uliopita.

Amesema chama cha CCM kimeingiwa na hofu kutokana na nguvu na umoja wa ACT Wazalendo licha ya changamoto zilizojitokeza wakati wa uchaguzi.

“Leo CCM wamepatwa na wasiwasi mkubwa. Licha ya kufanya uchafu katika uchaguzi uliopita, bado wanatuona tumesimama imara. Wameanza kujiuliza kuna nini ndani ya ACT Wazalendo,” amesema Othman.

Ameongeza kuwa umoja wa wanachama wa chama hicho ndio silaha muhimu ya kisiasa itakayowawezesha kukiondoa chama cha Mapinduzi (CCM) madarakani.

Kuhusu madai ya kuporwa kwa baadhi ya majimbo, Othman alisema chama chake kimefungua kesi katika Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa ajili ya majimbo 14 ya Pemba, na kwamba wameanza mchakato wa kudai haki kutokana na kile alichokiita “kubakwa kwa uchaguzi.”

Mapema, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Ismail Jussa, amesema kuwa mazungumzo yoyote yatakayofanyika lazima yahusishe kudai haki ya Wazanzibari, akisisitiza kuwa viongozi wa chama hawatachukua uamuzi wowote bila kuwashirikisha wanachama.

“Nawaombeni mtuamini sisi viongozi wenu. Chochote tutakachofikia kwenye mazungumzo, hatutaamua bila kurudi kwenu,” alisema Jussa huku akishangiliwa na wanachama.

Kwa upande wake, Katibu wa Jimbo la Wingwi, Abdalla Ali Said, alisema matukio yaliyoshuhudiwa katika uchaguzi uliopita yalikuwa kama “vituko vya watoto wachanga,” akidai kuwa baadhi ya mawakala wa chama hicho waliondolewa vituoni na kuachwa kwenye matope wakati wa mvua.

“Hawa jamaa hawawezi tena kufanya uchaguzi wa haki, bali kudanganya dunia,”amesema Abdalla.