November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Othman : Tutapambana na changamoto za elimu kwa maendeleo

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,  Othman Masoud Othman, amesema kuwepo kwa wingi wa changamoto katika Sekta ya Elimu, ni athari kwa jamii na maendeleo ya Nchi kwa ujumla.

Othman ameyasema hayo leo, mwanzoni mwa ziara yake ya kuzitembelea taasisi mbali mbali za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, inayoendelea katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Amesema kuwa wingi wa changamoto hizo unaathiri moja kwa moja utoaji na ustawi wa huduma katika jamii, hali inayoweza kuzorotesha azma na kasi ya maendeleo ya Nchi, kwa kuzingatia umuhimu wa kipekee wa sekta hiyo.

Akijionea miongoni mwa changamoto hizo, ikiwemo wingi wa wanafunzi katika madarasa ya Skuli ya Mtopepo, yenye takriban watoto 170 hadi 200 kwa baadhi ya kila darasa,  Othman ameeleza kuwa hapo ni kipimo cha mazuri na machungu ya upatikanaji wa huduma ya elimu hapa nchini, hasa kwa kujali namna walimu wanavyopambana kuifanikisha kwa mafanikio.

Othman amepongeza Walimu wa skuli hiyo, Wazazi, Kamati za Wazee na Uongozi wa Wizara ya Elimu kwa ujumla, kwa juhudi wanazozichukua zikiwemo za kujenga ufaulu wa wanafunzi, licha ya mazingira magumu yanayowazunguka.

Aidha, Othman ameeleza kuwa Mamlaka imeshazibaini changamoto hizo, na kuahidi kuchukua hatua za kuhamasisha utatuzi wake, akisema kuwa hiyo ni katika azma ya msingi ya kujumuika na kushirikiana katika Serikali iliyopo Zanzibar ya Umoja wa Kitaifa, ili kutekeleza mahitaji ya wananchi, ikiwemo kuwapatia huduma bora.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar,  Leila Mohamed Mussa, akiwasilisha Taarifa fupi ya Utekelezaji, iliyobainisha pia changamoto mbali mbali zikiwemo za uhaba wa vifaa, raslimali, walimu wa sayansi na ufinyu wa bajeti, ameeleza matumaini yaliyopo katika kufanikisha mageuzi ndani ya Mamlaka hiyo kuanzia Mwaka ujao wa Fedha wa 2022 – 2023, yakiwemo utekelezaji wa Mtaala Mpya wa Msingi na Maandalizi, na ufanikishaji wa Miradi mbali mbali, katika maendeleo ya sekta hiyo.

Katika ziara hiyo,  Othman ametembelea maeneo mbali mbali ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, ambayo ni pamoja na Ukaguzi wa Ujenzi wa Majengo Mapya ya Kisasa, katika Skuli za Mtopepo Juu, Mwanakwerekwe H na Bweleo, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Ziara hiyo imewajumuisha pia Viongozi, Wakurugenzi na Watendaji mbali mbali, akiwemo Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar,  Ali Abdulgullam Hussein, na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Ali Khamis Juma.