Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema serikali atakayoiongoza itazipa kipaumbele bidhaa zote zinazozalishwa visiwani humo, hususan zile zinazotokana na useremala na kazi za mikono, ili ziweze kushindana katika soko la kimataifa na kuinua uchumi wa wananchi.
Akizungumza wakati alipotembelea wajasiriamali na wauzaji wa furniture katika eneo la Mkokotoni, Othman amesema Zanzibar imekuwa ikitambulika kwa muda mrefu kwa kuzalisha bidhaa bora, zenye ubunifu wa kipekee na michoro ya kuvutia, lakini mifumo mibovu ya kiuchumi na ukosefu wa masoko umewafanya mafundi hao kubaki katika umasikini.
Amesema Zanzibar imekuwa ikitajwa kwa zama za zamani kwenye masuala ya useremala na ubunifu wa mikono, lakini leo mafundi wengi wako katika hali ngumu ya maisha kutokana na kukosekana kwa sera bora za uendelezaji wa sekta hiyo.
Othman amesema serikali ya ACT Wazalendo itahakikisha wajasiriamali wadogo wanapatiwa mikopo nafuu, elimu ya biashara, pamoja na fursa za mafunzo ya kisasa ili bidhaa zao ziweze kuingia katika viwango vya kimataifa.

Aidha, amesema serikali yake itaweka utaratibu wa masoko ya kimataifa ya bidhaa za asili za Zanzibar kama vile samani, vinyago, bidhaa za mwani, viungo na nguo zenye vionjo vya utamaduni wa Kizanzibari, ili kuimarisha uchumi wa wananchi wa visiwa hivyo.
Othman ameongeza kuwa Zanzibar ni kisiwa chenye utajiri mkubwa wa ubunifu na bidhaa za kipekee ambazo zinaweza kuwa chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana, wanawake na mafundi wa ndani ikiwa tu zitatunzwa, kutangazwa na kuwekewa sera madhubuti.

Amewahimiza wananchi kuwa na dhamira ya kweli ya mabadiliko kwa kumchagua kiongozi mwenye nia ya kuendeleza rasilimali zao na kuzitumia kwa manufaa ya wote.
Amesema Wazanzibari wanapaswa kuchagua kwa matumaini, sio kwa mazoea, na serikali ya ACT Wazalendo itahakikisha kila bidhaa inayozalishwa Zanzibar inapewa thamani na kufikishwa katika soko la kimataifa.

Ziara hiyo ya Othman Masoud imekuwa kivutio kikubwa kwa wakazi wa Mkokotoni, ambapo wengi walionyesha matumaini makubwa kwamba mabadiliko ya kweli ya kiuchumi yanawezekana chini ya uongozi wa ACT Wazalendo.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina