Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, amesema kuwa sasa dunia inashuhudia mabadiliko makubwa ambayo Jeshi la Polisi Nchini linapaswa kwenda nayo sambamba ili kukuza ufanisi.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo, Nyumbani kwake Chukwani, Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja, wakati akipokea salamu za kuagana kutoka kwa aliyekuwa Kamishna wa Polisi Zanzibar, Awadh Juma Haji.
Amesema kuwa miongoni mwa mabadiliko muhimu ni pamoja na maendeleo ya teknolojia na mbinu za kisasa za kuimarisha usalama katika mazingira yote, ambazo pindipo Jeshi hilo litazitumia, litajikuza kiuwezo hususan wa kukabiliana na uhalifu wa makosa mbali mbali.
“Nchi kama hii ya Zanzibar usiichukulie kwa udogo wake; hali ya ongezeko kubwa la watu, lakini kama ilivyo kwengineko duniani, wahalifu nao siyo tu wale wa kukimbizana, wanabadili mbinu za kila namna, hivyo kunahitajika ufanisi wa kukabiliana nao”, ameeleza Mheshimiwa Othman.
Mheshimiwa Othman pamoja na kumtakia kila la kheri katika majukumu ya sasa, amemtaja Kamanda Awadh kuwa ni mtu ambaye ni kama kwamba kwa upande wake Zanzibar imemfaa, na imekuwa ni sehemu muhimu ya kuvuka kuelekea hatua za juu zaidi kiutendaji, ndani ya Jeshi hilo.
Kwa upande wake Kamanda Awadh, ameshukuru maelekezo, miongozo na mashirikiano mema aliyopata kutoka kwa Viongozi wa Zanzibar, akiwemo Mheshimiwa Othman, akisema kwamba kwa kuthamini hilo ameonelea si vyema kwenda katika Kituo chake Kipya cha Kazi, ambacho ni Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Jijini Dodoma Tanzania Bara, bila ya kufuata tena njia ya kuonana na kuagana na Wakuu.
Hatua hiyo imekuja kufuatia Uteuzi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, na Mabadiliko ya Watendaji mbali mbali ndani ya Jeshi la Polisi, ambapo Kamanda Awadh ameteuliwa kuwa Kamishna Mpya wa Operesheni na Mafunzo.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato