December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Oryx Gesi yawashika mkono wajasiliamali 450 Tanga Mjini

Na David John, TimesMajira Online, Tanga

WAZIRI wa Afya ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini Ummy Mwalimu amekabidhi mitungi mikubwa ya gesi ya Oryx 150 pamoja na majiko yake bure kwa wanawake wajasiriamali 450 katika Jiji la Tanga.

Akizungumza leo jijini Tanga wakati akikabidhi mitungi hiyo iliyotolewa na Kampuni ya Oryx Gas kwa kushirikiana na Cocacola Waziri Ummy amewapongeza wadau hao kwa kutoa vifaa hivyo kwa wajasiriamali wanawake wa jiji hilo ambapo inakwenda kuwa msaada mkubwa sana.

Akikabidhi mitungi hiyo Waziri Ummy alitumia nafasi hiyo kueleza malengo ya Serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa itaendelea kuthamini na kutambua mchango wa wanawake pamoja na kuwashirikisha katika ngazi mbalimbali za maamuzi.

“Tunawashuku wadau wote kwa kutuunga mkono kwa kutupatia bure mitungi ya gesi Oryx na majiko yake,meza pamoja na kreti 150 za Cocacola kwa ajili ya wanawake wajasiriamali wa Tanga.

“Tunaamini matumizi ya nishati ya gesi yatakwenda kumaliza matumizi ya kuni na mkaa katika kupikia.Nitoe rai kwa wanawake hiki ambacho tumekipata leo iwe ni chachu ya kuboresha biashara zetu,”amesema Waziri Ummy

Aidha amewataka wajasiriamali hao wasijione wanyonge kwani wanaweza kufanya vizuri zaidi ya wanavyofanya sasa huku akifafanua kwa sasaa kuna watoto wengi wanamaliza vyuo na vyuo vikuu nafasi ya kuajiriwa ni chache.

“Kwa hiyo lazima tujiajiri na tuchukulie ujasiriamali kama ofisi rasmi, hivyo niendelee kuwaomba wanawake wajiamini na wajithamini katika kuimarisha biashara zenu.

Amesema Serikali ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan itaendelea kutambua na kuthamini mchango wa wanawake pamoja na kuwashirikisha wanawake katika nafasi za maamuzi.”

Awali akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kampuni ya Oryx Gas Benoit Araman , Meneja Masoko wa kampuni hiyo Kanda ya Mashariki Shaban Fundi amesema lengo la kutoa mitungi hiyo ya gesi ni kuendeleza kampeni yake ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia huku ikisisitiza pia Oryx gas imekua ikiyaishi maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kwamba ifikapo 2032 asilimia ya 80 ya watanzania watumie nishati safi ya kupikia.

Shaban amesema matumizi ya gas yamekua yakiongezeka kwa kasi nchini kutokana na juhudi kubwa ya kuhamasisha inayofanywa na Oryx Gas kwa kushirikiana na wadau ikiwemo Serikali inayoongozwa na Rais Samia.

“Kwa ushirikiano mkubwa uliopo kati ya OryxGas na Cocacola, tumeendelea kuwezesha makundi mbalimbali ya wajasiriamali hususani wanawake maeneo mbalimbali nchini katika kuhamasisha watanzania wengi watumie nishati safi ya kupikia, ” amesema.

Amefafanua kupika kwa Gas ya Oryx kunaimarisha afya kwa kuepuka kuvuta moshi mbaya wa kuni na mkaa,kupika kwa umaridadi na kwa wakati, hivyo kuongeza mapato mengi huku akikisitiza kwa ujumla ni pamoja na kulinda mazingira kwa kuzuia kukata miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Ameongeza hivyo Oryx imeendelea kuwekeza kuhakikisha nishati hiyo inapatikana nchini kote lakini zaidi wanawekeza katika kutoa elimu kupitia makundi mbalimbali kuhusu matumizi sahihi ya Gas

Pamoja na hayo amesema kwa ushirikiano na Cocacola hadi sasa wamefanikiwa kutoa mitungi ya gesi ya Oryx zaidi ya 2000 na kuwafikia wajasiriamali 5000 na wataendelea na ushirikiano kwa ajili ya kuyafikia makundi mengi zaidi ili kutimiza ndoto ya Rais Samia.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu (kushoto) na Meneja Masoko wa Oryx Gas Kanda ya Mashariki Shaban Fundi (kulia) wakiwa wameshika mtungi wa gesi wenye ujazo wa kilo 15 kabla ya kukabidhi kwa mmoja ya wanawake wajasiriamali katika Jiji la Tanga