Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online DSM
KAMPUNI ya Orixy Gas Tanzania kwa kushirikiana na Benk ya NMB, wameingia makubaliano ya kurahisisha upatikanaji wa huduma ya gesi safi ya kupikia kuiunga mkono serikali katika mapambano ya uharibifu wa mazingira.
Kutokana na hatua hiyo, wananchi watakaonunua mitungi ya gesi ya kampuni ya Oryx watapata punguzo maalumu kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akizungumza katika hafla fupi ya utiaji saini makubaliano hayo iliyofanyika Leo Novemba 27,2023 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania (OGTL), Benoit Araman, Amesema anaamini kuwa ushirikiano Taasisi ya fedha ya NMB ni wa kimkakati katika kuhakikisha ufumbuzi wa nishati safi ya kupikia unapatikana kwa kila mwananchi.
“Mtandao wetu wa usambazaji pamoja na uhamasishaji mkubwa kutoka kwa NMB utaleta hatua nyingine muhimu kwa Watanzania kupata bidhaa zetu kwa urahisi, haraka na ufanisi mkubwa “Amesema
Araman amefafanua kuwa kwa miaka mingi OGTL imekuwa ikiongoza jitihada za kukuza matumizi ya gesi nchini, ambapo hivi karibuni kuanzia mwaka 2021 kampuni hiyo imekuwa ikiratibu juhudi za kuunga mkono ajenda ya serikali iliyoidhinishwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya matumizi Nishati safi ili kulinda mazingira.
“Rais Dkt Samia ametoa maelekezo kuwa ifikapo mwaka 2032, asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia na Leo tunashuhudia mdau mwingine (NMB) akiungana nasi katika kufanikisha azma hii ya Rais wetu na ndoto ya Watanzania kupikia Nishati safi na Salama,” amesema.
Akizungumzia zaidi kuhusu Kampuni hiyo Araman Amesema kampuni hiyo ina wasambazaji na maduka ya kutoa huduma ya gesi nchi nzima ambayo hivi sasa yatakuwa tayari kuwahudumia wateja wote wa NMB ambao watakuwa wakitumia kadi zao za benki au huduma nyingine za kufanya malipo ya kulipia gesi.
Naye Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi , amesema kuwa makubaliano hayo yanaendana na mkakati wa Benki hiyo inavyounga juhudi za serikali za kutunza mazingira kupitia matumizi ya NIshati salama na safi ya kupikia .
Mponzi amesema kuwa hata hivyo wao kama NMB mapema mwaka huu wamezindua mkakati wa kupanda miti bilioni moja nchi nzima ambao utekelezaji wake unaendelea na lengo ni kuhakikisha mazingira yanatunzwa kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Amesema bodi ya NMB iliidhinisha fedha hizo kiasi cha sh. bilioni mbili katika bajeti ya mwaka huu wa fedha ambazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa katika shughuli mbalimbali za kutunza mazingira hapa nchini .
“Tunawahakikishia Watanzania kuwa tumedhamiria kuimarisha utunzaji wa mazingira, kupitia makubaliano haya tutatoa ofa ya punguzo la gharama za gesi kwa mitungi ya viwango mbalimbali inayouzwa kupitia kampuni ya Oryx Gas Tanzania.
Mmoja wananchi mkazi wa Mtaa wa Ufipa, Kinondoni, Dar es Salaam, Mwanahawa Mfaume, akizungumzia makubaliano hayo amepongeza hatua hiyo kwa kuwa yatawasaidia kupunguza gaharama za gesi.
Mwanahawa amesisitiza kuwa iwapo mitungi ya gesi itapatikana kwa bei himilivu na kujazwa kwa gaharama nafuu, itawahamasisha wananchi wengi kutumia huduma hiyo na kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa kama iiivyozoeleka.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi