November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Oryx Gas, Dkt. Mwigulu wamwaga mitungi, majiko Iramba Magharibi

Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline,Iramba

KAMPUNI ya Oryx Gas Tanzania kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi ambaye pia ni Waziri wa Fedha Dkt.Mwigulu Nchemba, wamegawa mitungi ya gesi ya gesi ya Oryx 700 pamoja na majiko yake kwa wananchi na wajasiriamali wakiwemo Baba na Mama Lishe.

Akizungumza jana wakati wa ugawaji wa mitungi hiyo uliohudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Seleman Mwenda, Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania, Benoit Araman ameendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Pia amewaomba Watanzania kuyatazama matumizi ya gesi ya kupikia nyumbani kuwa huduma muhimu na mwafaka katika kulinda afya ya jamii.

“Oryx Gas tunaamini ukipika kwa gesi ya Oryx utakuwa unalinda mazingira kwa kuacha kukata kuni na mkaa, lakini utakuwa unalinda afya ya wanawake kwa kuwaepusha kuvuta moshi na mvuke unaoathiri mapafu na afya yao unaotokana na kuni na mkaa.

“Wanawake wanatumia muda mchache kupika kwa gesi na hivyo wanapata nafasi kufanya shughuli nyingine za maendeleo na kuepuka kugombana na wenza wao kwa kuchelewesha chakula,” amesema.

Pia amesema kupika kwa kutumia gesi ya Oryx, watoto wanapata muda mwingi wa kusomea na sio kwenda kutafuta kuni huku akisisitiza kutumia mtungi wa gesi ya Oryx pia kunamaanisha kulinda na kuboresha maisha ya wanawake kwa kuwazuia kwenda kukusanya kuni msituni.

Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania, Benoite Araman (kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Iramba Seleman Mwenda ( wa pili kushoto) wakimkabidhi mtungi wa gesi wa Oryx Mama Lishe, Sada Said (katikati) wakati wa hafla ya ugawaji mitungi uliofanywa kwa wananchi 700 wa Wilaya hiyo wakiwemo wajasiriamali pamoja na Baba na Mama Lishe. Na mpiga picha Wetu.

“Kwa miaka mingi Oryx Gas imekuwa kampuni kiongozi katika kukuza matumizi ya gesi nchini. Kuanzia Julai mwaka 2021 tumekuwa mstari wa mbele kutekeleza maelekezo ya Serikali tulioyapokea kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa ifikapo mwaka 2032 asilimia 80 ya wananchi watumie nishati safi ya kupikia,” amesema.

Amesisitiza kupitia mipango hiyo, Oryx Gas inataka kutokomeza matumizi ya nishati chafu ya kuni na mkaa ambayo si tu mbaya kwa afya bali pia ni hatari kwa mazingira.

Pia, alimshukuru Dkt. Nchemba kuwa balozi mzuri wa kuleta maendeleo kwa wanawake na jamii kwa ujumla kwa kuiunga mkono Oryx Gas Tanzania katika mpango wa matumizi ya nishati safi mkoani Singida.

“Tunafurahi kumkabidhi mitungi ya gesi 700 kwa wakazi wa Iramba yenye thamani ya sh. milioni 50,”amesema Benoite.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iramba mkoani Singida Seleman Mwenda aliyemwakilishia Dkt. Mwigulu amelisema jitihada za kuhamasisha nishati safi ya kupikia kwa kugawa mitungi ya gesi ya Oryx ni sehemu za kumuunga mkono Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuhimiza wananchi kutumia nishati safi ya kupikia.

“Kupika kwa gesi kunasaidia kutunza mazingira pamoja na afya hasa kwa baba na mama lishe ambao wanajihusisha na shughuli za upishi kwani tumegundua misitu mingi inateketea kwa sababu ya matumizi ya kupikia,”alisema.

Pia amesema athari nyingi ambazo wanazipata baba na mama lishe zinatokana na mkaa pamoja na kuni na hivyo kuathiri afya zao.

“Katika kuunga mkono juhudi za Serikali tuliamua kuwasiliana na Oryx na tunashukuru wameitikia mwito uliopelekekwa na Mbunge wetu na Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba…

“Tumeungana kuhakikisha wananchi wa Iramba wanaingia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ambayo inafaida nyingi ikiwemo kuokoa muda wa kupika chakula maana sio lazima kuandaa moto.

“Kupika kwa gesi kunaokoa muda kwa watoto wanaoshindwa kwenda shule wakati mwingine kwa ajili yaa kwenda kuokota kuni na kuandaa mkaa.Pia tunaokoa mazingira yetu kwa sababu ya kukata miti kwa ajili ya kuni na kuandaa mkaa.Kwahiyo matumizi ya gesi yanakwenda kuondoa tatizo hilo.”