January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Operesheni maalum,kufanyika Ziwa Victoria

Na Judith Ferdinand ,Timesmajira Online, Mwanza

Igombe,Kata ya Bugogwa wilayani Ilemela,mkoani Mwanza,Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza,limefanya uzinduzi wa oparesheni maalumu ndani ya Ziwa Victoria,lengo ni kuimarisha mifumo ya kiusalama.

Miongoni mwa waliohudhuria uzinduzi huo ni Thadeo Philip maarufu Bonge,mmoja wa wakazi wa Igombe,ambaye ameeleza kuwa,kipindi cha nyuma maeneo hayo yalikuwa na uhalifu wa kutumia silaha.Lakini tangu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,DCP.Wilbord Mutafungwa,amehamishiwa mkoani Mwanza, hawajawahi kusikia bunduki inalia Igombe.

Juma Kavilondo,naye ni mwananchi wa Kata ya Bugogwa,amekiri kuwa,uhalifu wa kutumia silaha Ziwa Victoria,umekuwa historia kwani Jeshi la Polisi limefanikiwa kudhibiti.

“Ujambazi wa kutumia silaha, sijauona kwa muda mrefu labda ni matukio baadhi tu ya udokozi,”amesema Kavilondo.

Uzinduzi wa oparesheni maalumu ndani ya Ziwa Victoria ulienda sambamba na utoaji elimu ya usalama majini na ukatili wa kijinsia,ilioyolewa na Mkuu wa Kikosi cha Wanamaji Mkoa wa Mwanza Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Wenceslaus Muchunguzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,DCP. Wilbrod Mutafungwa,Agosti 20, 2024 katika mwalo wa Igombe, Kata ya Bugogwa Wilaya ya Ilemela,akizungumza na uongozi wa Serikali za Mitaa na wananchi,amesema,wameendelea na jitihada za kuimarisha mifumo ya kiusalama na kutokomeza vitendo vya kihalifu katika fukwe, mialo na visiwa ndani ya Ziwa Victoria kwa kuishirikisha jamii.

DCP.Mutafungwa pia amezindua awamu nyingine ya kusikiliza kero za kiusalama kutoka kwa wananchi.”Siku ya leo,nimekuja kuzindua awamu nyingine ya kusikiliza kero, changamoto, malalamiko na kupata ushauri kutoka kwa wananchi,”.

Pia amewaasa, wananchi wa Kata ya Bugogwa kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi,kuzuia uhalifu kuanzia ngazi ya familia kwani jukumu la ulinzi na usalama ni la jamii nzima.

Sanjari na hayo,DCP Mutafungwa,amepita katika Soko la kimataifa la samaki na dagaa lililopo Mwaloni Kirumba Kata ya Kirumba wilayani Ilemela,na kutangaza operesheni ya kuwasaka wahalifu katika maeneo yote yaliyopo pembezoni mwa ziwa Victoria na visiwa vya Mkoa wa Mwanza.