Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Katika kipindi cha wiki moja Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa zaidi ya 300 wanatuhumiwa kuhusika na makosa mbalimbali.
Akizungumza jijini hapa Januari 26,2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa ameeleza kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa kufuatia operesheni inayoendelea mkoani humo huku akitaja Wilaya zilizoongoza kuwa na idadi kubwa ya wahalifu kuwa ni Nyamagana, Ilemela na kwa kiasi kingine kikubwa ni Wilaya ya Magu pamoja na Misungwi.
Mutafungwa ameeleza kuwa jumla ya watuhumiwa 335 wamekamatwa ambapo watuhumiwa 133 wamehojiwa na kufikishwa mahakamani na watuhumiwa 202 bado wanaendelea kuhojiwa na upelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Ameeleza kuwa hiyo ni mafanikio ambayo jeshi hilo imelipata kutokana na misako mbalimbali inayoendelea dhidi ya watu wanaojihusisha na matukio ya kihalifu ili kuwaepusha wakazi wa Mkoa wa Mwanza na wimbi la uhalifu unaoweza kusababisha hofu kwa wananchi hivyo kuwafanya wasifanye kazi mbalimbali za kuwaletea maendeleo yao au wasifanye shughuli mbalimbali za kijamii kwa kuhofia wahalifu.
“Kutokana na misako hiyo ambayo itakuwa endelevu tumepata mafanikio ya kuzuia na kudhibiti matukio ya kihalifu katika maeneo mbalimbali,baada ya kuwatia mbaroni washukiwa mbalimbali wa matukio ya kihalifu katika operesheni hiyo ya wiki moja,”ameeleza Mutafungwa.
Hata hivyo ametaja idadi ya watuhumiwa wa kujihusisha na vitendo vya uhalifu 47, kuingia nchini bila kibali 5, watuhumiwa wa wanaojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya 51, watuhumiwa wa mauaji 13 na watuhumiwa wa kuvunja nyumba na kuiba 17.
Sanjari na hayo ameeleza kuwa
Miongoni mwa vielelezo vilivyokamatwa katika operesheni hiyo ni simu za mkononi za aina mbalimbali zaidi ya 50, dawa za kulevya aina ya mirungi, misokoto ya bhangi, na vifaa vya kufanyia uhalifu pamoja na mali zilizoibwa sehemu mbalimbali katika makazi ya watu.
Hivyo amewaomba wananchi kuendelea kufichua matukio ya kihalifu katika jamii ili waweze kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wote watakao bainika huku akitoa onyo kali kwa wahalifu popote walipo kwani wapo imara na wataendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wahalifu kwa kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
“Taarifa kuhusu wahalifu na uhalifu zimeendelea kupatikana kutokana na ukusanyaji wa taarifa fiche zinazohusu wahalifu, kazi inayofanywa kwa weledi mkubwa na askari wetu, taarifa nyingine tumeendelea kuzipata kutoka kwa wananchi wasiopenda uhalifu na kupitia ushirikishwaji mkubwa wa jamii unaofanywa na jeshi la Polisi kupitia mikutano yake na wananchi inayoendelea kufanyika katika kata mbalimbali na kupata mafanikio makubwa katika kuwafichua wahalifu katika mitaa mbalimbali,”ameeleza Mutafungwa.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote