


Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza ongezeko kubwa la idadi ya wapiga kura waliojiandikisha kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ikiwa ni matokeo ya mafanikio ya zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumza jijini Dodoma katika hafla ya Uzinduzi wa Kalenda ya Uchaguzi Mkuu, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele, ameeleza jumla ya wapiga kura waliojiandikisha ni milioni 37.655 ikiwa ni ongezeko la asilimia 26.55% kutoka wapiga kura milioni 29.754 waliokuwepo mwaka 2020.
“Kati ya hao milioni 36.650 ni kutoka Tanzania Bara, huku Zanzibar ikiwa na wapiga kura milioni 1.0 Idadi hii inaonesha mwitikio chanya wa wananchi kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia,” amesema Jaji Mwambegele.
Kwa upande wa Zanzibar, ilielezwa kuwa wapiga kura 725,876 wako katika Daftari la ZEC, huku wengine 278,751 wakiwa wameandikishwa na INEC baada ya kukosa sifa za kujiandikisha kupitia ZEC.
Vituo vya kupigia kura vilivyopangwa kwa mwaka 2025 ni 99,911, ongezeko la asilimia 22.49% ikilinganishwa na 81,567 vya mwaka 2020.
Aidha amesema,uboreshaji wa daftari la mpiga kura unafanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza zoezi hilo lilifanyika kati ya Julai 20, 2024 – Machi 25, 2025 hulu awamu ya pili zoezi lilifanyika kati ya Mei 1 – Julai 4, 2025.
“Katika kipindi hicho,wapiga kura wapya mulioni 7.6 waliandikishwa (asilimia 136.79 ya makadirio ya awali) na milioni 4.29 waliboresha taarifa zao , wapiga kura 99,744 waliondolewa kwenye daftari kwa kupoteza sifa, wapiga kura 8,703 walibainika kujiandikisha zaidi ya mara moja na taarifa zao zimekabidhiwa kwa Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi za kisheria.”amesema Jaji Mwambengele
Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) inaendelea na uchakataji wa daftari la wapiga kura kwa mujibu wa sheria, na wadau watajulishwa iwapo kutakuwa na mabadiliko yoyote ya takwimu.
Aliwapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi, pamoja na vyama vya siasa, asasi za kiraia, na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha zoezi hilo kwa kutumia fedha za ndani.
“Tume inawashukuru wadau wote kwa ushirikiano wao na itaendelea kusimamia uchaguzi kwa haki, uwazi, na kwa mujibu wa sheria,” alisisitiza.
Ratiba ya Uchaguzi Mkuu 2025
Kwa mujibu wa mamlaka ya kikatiba na kisheria chini ya ibara ya 41(4) ya Katiba ya 1977, pamoja na Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya 2024, INEC imetangaza ratiba rasmi ya uchaguzi kama ambapo Agost 9 – 27, 2025 ni utoaji wa fomu za uteuzi wa wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais,Agosti 14 – 27, 2025 ni utoaji wa fomu za uteuzi wa wagombea wa Ubunge na Udiwani.
Vile vile amesema Agosti 27 , 2025 ni siku ya Uteuzi wa wagombea wa nafasi zote,Agosti 28 hadi Oktoba 28 Oktoba, 2025 no kampeni za Uchaguzi kwa Tanzania Bara,Agosti hadi Ojtoba 27 , 2025 ni Kampeni za Uchaguzi kwa Tanzania Zanzibar ili kupisha kura ya mapema na Oktoba 29, 2025 (Jumatano) itakuwa ni Siku rasmi ya Kupiga Kura.
Hatua Dhidi ya Wapiga Kura Waliokiuka Sheria
Mkurugenzi wa Uchaguzi Ramadhan Kailima alikabidhi rasmi orodha ya watu 8,703 waliojiandikisha zaidi ya mara moja kwa Jeshi la Polisi.
Taarifa hiyo ni sehemu ya kalenda ya uchaguzi, na hatua za kisheria zitaendelea kuchukuliwa kwa mujibu wa Kifungu 114 cha Sheria ya Uchaguzi, ambacho kinaainisha adhabu kwa makosa hayo.
Ametoa wito kwa wananchi na wadau wote kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi kwa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo, na maelekezo yatakayotolewa na Tume katika kipindi chote kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi