November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Okumu ajigamba kuendeleza ushindi Biashara United

Na Fresha Kinasa, TimesMajira Online, Mara

KOCHA mpya wa timu ya Biashara United ya Mara Patrick Odhiambo Okumu ameahidi kuendeleza mazuri yaliyofanywa na watangulizi wake ikiwemo kupata ushindi katika kila mchezo ulio mbele yao.

Kocha huyo raia wa Kenya mwenye leseni B ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) jana ametambulishwa rasmi kurithi mikoba ya Francis Baraza aliyetimkia Kagera Sugar baada ya kusaini kandarasi ya miaka miwili.

 Mara baada ya Baraza kuondoka, uongozi wa Biashara ulianza haraka mchakato wa kumsaka kocha mkuu huku wakiamua timu kuikabidhi kwa kocha msaidizi Marwa Chambeli ambaye amefanikiwa kuendelea kuibakiza timu hiyo katika nafasi ya nne hadi sasa katika msimamo wa Ligi wakiwa na pointi 44.

Lakini pia kocha huyo amefanikiwa kuipeleka timu hiyo katika hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam ‘Azam Sports Federation Cup’ baada ya ushindi wa penalti 4-1 dhidi ya Maafande wa Ruvu Shooting baada ya dakika 90 za mchezo huo kumalizika kwa sare ya goli 1-1.

Akizungumza mara baada ya kutambulishwa, kocha huyo aluyewahi kuzinoa timu za Kaka Mega Home Boys, Gor Mahia na Sony Sugar amesema kuwa, kazi yake kubwa ni kuendeleza mazuri yaliyofanywa na kocha Baraza pamoja na wasaidizi wake.

Okumu amesema kuwa, siku zote ili kufanikiwa katika soka basi ni lazima timu iwe na lugha moja hivyo ili kupata kile anachokihitaji ni lazima benchi la ufundi liwe kitu kimoja katika kutelekeza majukumu yao.

“Nashukuru kwa kupata mapokezi mazuri hivyo ninaahidi nitaendeleza yale mazuri waliyoyafanya kina kocha kocha Baraza kwani ninaamini ili kufanikiwa ni lazima tuzungumze lugha moja hivyo nitahakikisha natelekeza majukumu yangu kwa ufanisi mkubwa,” amesema kocha huyo.

Akizungumza wakati wa kumtambulisha kocha huyo, Mwenyekiti wa Biashara, Seleman Mataso amesema kuwa, wameamua kumleta Mkenya kutokana na falsafa yake kuendana na ile aliyokuwa akiitumia kocha Baraza.

“Tumepokea maombi mengi sana kutoka kwa makocha tofauti lakini tukaamua kumpitisha Okumu kutokana na falsafa ya mtangulizi wake kuwa nzuri hivyo tunaamini atatufikisha tunapotaka, uongozi utampa ushirikiano anaouhitaji ili kuweza kutufikisha pale tunapopahitaji,” amesema Mataso.