November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ofisi ya Taifa ya Mashtaka yashauriwa kuboresha majengo yake nchini

Na Suleiman Abeid,
Timesmajira Online, Shinyanga

OFISI ya Taifa ya Mashtaka imeshauriwa kuendelea kuboresha zaidi majengo ya ofisi zake katika mikoa mbalimbali nchini ili kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa wadau wake na wananchi kwa ujumla.

Hali hiyo imeelezwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Khatibu Kazungu wakati wa ufunguzi wa jengo la ofisi ya Mashtaka mkoani Shinyanga ambapo amesema mazingira salama, rafiki na wezeshi ya kazi kwa watumishi ni chachu ya utekelezaji bora wa majukumu yao.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria Dkt.Khatibu Kazungu

Dkt. Kazungu amefafanua kuwa ni wakati muafaka wa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini kuwa na mipango madhubuti na endelevu ya kubuni na kusimamia miradi ya ujenzi wa majengo ya ofisi ili kuongeza ubora wa utoaji huduma kwa wadau.

“Nimearifiwa kuwa jumla ya miradi kumi na tatu ya ujenzi wa ofisi inatekelezwa, kati ya miradi hiyo, mradi mmoja ni ujenzi wa ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu na miradi kumi na moja ni ujenzi wa ofisi mpya za mikoa,”amesema na kuongeza;

“Pia mradi mmoja ni wa ukarabati ambapo kati ya hiyo, miradi sita imekamilika na miradi saba inaendelea kutekelezwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.rai yangu mikakati ya uboreshaji wa mazingira ya kazi kwa watumishi mliyoianza iendelezwe,” ameeleza Dkt. Kazungu.

Ameendelea kueleza kuwa Ofisi ya Mashtaka ni muhimu katika kuhakikisha haki, amani na usalama vinatamalaki kwa maendeleo ya taifa kwa kuboresha mnyororo wa utoaji wa haki jina.

Huku wajibu uliopo mbele ya watendaji ni kuhakikisha wanalinda na kusimamia vyema tunu na raslimali za Taifa.

Boniface Butondo (MB) mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Utawala, Katiba na Sheria

“Namshukuru Rais kwa nia yake ya dhati ya kuleta mageuzi makubwa katika sekta hii ya Haki Jinai, mageuzi haya yana lengo la kuhakikisha mfumo wa utoaji haki jinai unaboreshwa kwa lengo la kuwanufaisha watanzania wote,” ameeleza Dkt. Kazungu.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge, Utawala, Katiba na Sheria, Boniface Butondo ambaye ni mbunge wa Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga amesema Kamati yao imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa u

“Huu ni mhimili ambao tunautarajia sana katika kuimarisha na kujienga amani ya Tanzania, tunakushukuru Mkurugenzi kwa kuungana bega kwa bega na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha unasimamia fedha za maendeleo na hasa katika kuhakikisha kwamba miradi yote inayotekelezwa inatekelezwa katika kiwango bora,” ameleeza Butondo.

Naye mwakilishi wa Mkuu wa mykoa wa Shinyanga, Joseph Mkude ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kishapu amesema suala la haki jinai na utawala bora vinapaswa kupewa nafasi kubwa nchini na kwamba ili vifanikiwe lazima pawepo na vitendea kazi vya kutosha kwa wadau wanaosimamia.

Jengo jipya la Ofisi ya Mashtaka mkoani Shinyanga

Awali kwenye taarifa yake kwa mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Sylvestar Mwakitalu amesema katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa ofisi katika mikoa na wilaya ofisi yake hivi sasa imeanza mkakati wa ujenzi wa ofisi kwa mikoa kumi pamoja na makao makuu.

Mwakitalu ameitaja mikoa ambako tayari ujenzi unafanyika kuwa ni pamoja na Ilala, Pwani, Morogoro, Mbeya, Shinyanga, Njombe, Katavi, Rukwa, Manyara na Geita ambapo kati ya ofisi hizo tayari majengo sita yamekamilika na yapo tayari kutumika.

Baadhi ya watumishi wa ofisi ya Mashtaka mkoani Shinyanga wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa Jengo jipya la ofisi ya Mashtaka la Mkoa.