Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
SERIKALI imesema,katika kuimarisha upatikanaji haki na utawala bora, Serikali kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Sekta ya Sheria, Namba 11 ya 2023 ilifanya marekebisho ya muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuanzisha Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria.
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt.Damasi Ndumbaro ameyasema hayo Leo Aprili 30,2025 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Alisema lengo la maboresho hayo ni kuongeza tija na ufanisi katika shughuli za uandishi wa sheria, urekebu na ufasiri wa sheria.
Kwa mujibu wa Dkt.Ndumbaro,muundo wa kiutawala wa Ofisi hiyo uliidhinishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo 14 Januari, 2025 ili kuiwezesha kuendelea kutekeleza majukumu yake.
Aidha alisema , tayari Ofisi imepewa fungu la kibajeti ambalo ni Fungu 101 kwa ajili ya kuiwezesha Ofisi hiyo kuandaa Mpango na Bajeti kila mwaka.
Vile vile alisema,Wizara kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (OMMS) imeendelea kuhakikisha kuwa sheria za nchi zinakwenda na wakati na zinaakisi sera na vipaumbele vya Serikali katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, kimazingira na kiteknolojia.
Dkt.Ndumbaro alisema,katika kipindi cha Julai, 2024 hadi Aprili, 2025 Ofisi iliandaa Miswada ya sheria 16.
Alieleza kuwa katika kipidi hicho, Wizara kupitia OMMS ilisimamia utangazaji wa Sheria Kuu mpya 15 ambazo zilisainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali .
Kwa mujibu wa Dkt.Ndumbaro,katika kipindi cha Julai, 2024 hadi Aprili, 2025, Wizara kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilihakiki na kuchapisha jumla ya Sheria Ndogo 903, ikilinganishwa na Sheria Ndogo 885 zilizohakikiwa na kuchapishwa katika kipindi kama hicho Mwaka 2023/2024.
“Lengo la kutengenezwa kwa sheria ndogo ni kufafanua maudhui yaliyobainishwa kwenye Sheria Kuu. Sheria hizo zinajumuisha Kanuni 125, Amri 171, Notisi 408, Sheria Ndogo 182, Matamko tisa na Hati nane.
Pia alisema ,katika mwaka 2024/2025, jumla ya Sheria Ndogo Kifani 40 ziliandaliwa kwa ajili ya kuziongoza Wizara, Taasisi na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika uandaaji wa Sheria Ndogo.
“Sheria zilizoandaliwnajumuisha Sheria 32 za Wizara na Taasisi za Serikali na nane za Halmashauri,aidha, Sheria Ndogo Kifani zinaandaliwa kwa ajili ya kuingizwa katika Mfumo wa kielektroniki wa OAGMIS ili kupunguza dosari za uandishi pamoja na kurahisisha mchakato wa uhakiki. “alisisitiza
Alilieleza Bunge kuwa kati ya Sheria hizo, Sheria nane zimekamilika na zimewekwa kwenye Mfumo wa OAGMIS baada ya kuhakikiwa na kuanza kutumika 01 Machi, 2025.
Katika hatua nyingine Waziri huyo alisema,katika kutekeleza programu ya kutumia lugha ya Kiswahili kwenye utoaji haki na kuwawezesha wananchi kuzielewa Sheria za nchi, Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa Sheria zote za nchi zinapatikana katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza.
Alisema huo ni utekelezaji wa Sheria ya Tafsiri ya Sheria Sura ya kwanza mapitio ya Mwaka 2021 inayoelekeza kutafsiri sheria zote zilizopo katika lugha ya Kiingereza kuwa katika lugha ya Kiswahili.
Hivyo alisema, katika kipindi cha Julai, 2024 hadi Aprili, 2025,
Wizara kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imekamilisha uhakiki wa mwisho wa Sheria Kuu 300 kati ya 446zilizotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili. Dkt.
Dkt.Ndumbaro alisema,katika kuhakikisha kuwa sheria zote za nchi zinaendana na wakati na kuwarahisishia watumiaji katika kufanya rejea ya sheria husika hususan wakati wa utoaji wa haki na utekelezaji wa wajibu ikiwemo huduma za kimahakama na ukusanyaji mapato, Wizara kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imekamilisha urekebu wa Sheria Kuu 446 za nchi na kuandaa Toleo la Sheria Zilizofanyiwa Urekebu la Mwaka 2023.
“Zoezi hili limefanyika kwa mujibu wa Sheria ya Urekebu wa Sheria, Sura ya nne toleo hili ni la pili tangu Nchi yetu ilipopata uhuru.
“Aidha, kwa kuzingatia uzito na umuhimu wa urekebu wa sheria, Toleo hili lilizinduliwa na Dkt. Samia , kwa hafla maalum iliyofanyika tarehe 23 Aprili, 2025 Ikulu-Chamwino. Toleo hili litaanza kutumika tarehe 1 Julai, 2025.
“Hatua hii ni sehemu ya jitahada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha utawala bora, utawala wa sheria na kuimarisha misingi ya utoaji haki.
Vilevile alisema,Wizara kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, imeendelea kushiriki na kutoa ushauri wa kisheria katika majadiliano mbalimbali ya mikataba ya kibishara, mikutano ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Alisema,katika kipindi cha Julai, 2024 hadi Aprili, 2025 jumla ya Mikataba ya Kitaifa na Kimataifa 2,574 kutoka Wizara, Idara zinazojitegemea, Mashirika ya Umma, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ilifanyiwa upekuzi ikilinganishwa na Mikataba 1,280 iliyofanyiwa upekuzi katika kipindi kama hicho mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la asilimia 101.
Dkt.Ndumbaro alisema,ongezeko hili linatokana na juhudi za Serikali kuongeza idadi ya miradi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi na miradi inayofadhiliwa na Wadau wa Maendeleo.
Aidha alisema, Hati za Makubaliano 514 zilifanyiwa upekuzi katika kipindi husika ikilinganishwa na 341 zilizofanyiwa upekuzi katika kipindi kama hicho mwaka 2023/2024. Alisema,ongezeko hili linaakisi jitihada za Serikali kuhamasisha uwekezaji na diplomasia ya ushirikiano wa kikanda na kimataifa.
More Stories
Mpango ujenzi wa nyumba ya Katibu Jumuiya ya wazazi kuanzishwa
Waandikishaji wapiga kura watakiwa kuzingatia weledi
CCM Songwe yatoa onyo kwa makada wanaojipitisha kabla ya kampeni