


Ofisi ya AG yatambua mchango wa wahariri katika kuelimisha umma
Na Joyce Kasiki,Timesmajira online Dodoma
NAIBU Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel Maneno, amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) inatambua na kuthamini nafasi ya Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini, ikiwaita “Askari wa Kalamu” kwa mchango wao mkubwa katika kuelimisha, kulinda na kusimamia masuala ya kijamii, hasa yale yanayohusu misingi ya Sheria na Utawala Bora.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wahariri wa Vyombo vya Habari kilichofanyika jijini Dodoma 11 Septemba 2025, Maneno amesema kuwa vyombo vya habari ni kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi, hivyo wahariri wanapaswa kuwa na uelewa wa kina wa masuala ya kisheria ili kuripoti kwa usahihi na bila kupotosha umma.
“Sisi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, tunaamini kuwa nyinyi Wahariri wa Vyombo vya Habari ni Askari wa Kalamu, kama tulivyo sisi Mawakili wa Serikali. Mna jukumu la kulinda misingi ya Utawala Bora kwa kutoa taarifa sahihi kwa wananchi,” amesema Maneno.
Ameongeza kuwa kikao hicho ni jukwaa muhimu kwa Wahariri kupata maarifa ya kutosha kuhusu majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kupitia mada zitakazowasilishwa kuhusu maeneo ya Ushauri wa Kisheria, Uandishi wa Sheria, pamoja na Majadiliano na Upekuzi wa Mikataba.
“Ni matarajio yetu kuwa mtatumia kikao hiki kutoa maoni yenu yatakayosaidia katika uelimishaji wa umma kupitia taarifa sahihi, hivyo kusaidia kupunguza upotoshaji unaoweza kujitokeza kwenye masuala ya kisheria,” ameongeza.
Katika maelezo yake, Maneno pia amebainisha kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaendelea na maboresho ya sheria mbalimbali ili ziendane na mahitaji ya sasa ya kijamii na kiuchumi, sambamba na mwelekeo wa Taifa kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
“Kwa upande wetu, tunatekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwa weledi na ufanisi, kwa kuhakikisha sheria zilizopo zinaoanisha na mwelekeo wa nchi kuelekea Dira 2050,” amesema Maneno.
Kwa upande mwingine, akizungumza kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Serikali, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Rodney Thadeus amewahimiza wahariri kutumia kikao hicho kujifunza kwa kina masuala ya kisheria ili waweze kuandaa taarifa zenye ukweli, usahihi na manufaa kwa taifa.
“Ndugu zangu Wahariri, tuendelee kusimamia misingi ya taaluma yetu kwa weledi ili kuhakikisha tunaripoti taarifa kwa usahihi unaotakiwa,” amesema Rodney.
Kikao hicho cha siku mbili kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wahariri wa Vyombo vya Habari kinatarajiwa kuhitimishwa 12 Septemba 2025, kikiwa na lengo la kuimarisha mahusiano na uelewa wa pamoja kuhusu masuala ya kisheria nchini.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina