December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ofisa TAKUKURU ‘feki’ atiwa mbaroni Dodoma

Na Mwandishi Wetu

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma inamshikilia, Simon Jumbe (43) mkazi wa eneo la Kisasa Jijini Dodoma kwa tuhuma za kujifanya Ofisa wa TAKUKURU kinyume na Kifungu cha 36 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Marejeo ya mwaka 2018.

Taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo, ilieleza kwamba mara kadhaa tumewataka wakazi wa Dodoma kuwakataa na kutoa taarifa za matapeli au watu wanaojiita maofisa wa TAKUKURU ambao wamekuwa wakiichafua Taasisi hiyo kwa vitendo vyao ambavyo ni kinyume na maadili ya utendaji wa TAKUKURU.

“Katikati ya Aprili mwaka huu, tulipokea taarifa kwamba mtuhumiwa Jumbe anajiita Ofisa wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma na kwamba amekuwa na tabia ya kuwalaghai watu na kuwadai fedha akisingizia kwamba atawasaidia kupata ajira ndani ya TAKUKURU na ofisi zingine za Serikali,” imeeleza taarifa.

Taarifa hiyo imeeleza kwamba ufuatiliaji wao umeonesha mtuhumiwa alimwahidi kaka wa mtoa taarifa wao kazi ya udereva ndani ya TAKUKURU na baada ya mtu huyo kumweleza kwamba hana leseni ya udereva daraja C, ndipo mtuhumiwa akataka apewe sh. 350,000 ili amsaidie kupata leseni.