October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza jambo na wafanyakazi wa Benki ya CRDB (hawapo pichani) wakati wa ufungunzi wa mafunzo ya ushirikiano kati ya Wizara ya Madini na benki hiyo iliyofanyika Agosti 6, 2020 jijini Dodoma. (Picha na WM).

Nyongo azitaka benki kushirikiana na wizara katika kukuza uchumi wa madini

Nuru Mwasampeta na Steve Nyamiti,WM

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo azitaka benki zilizopo nchini kushirikiana na Wizara ya Madini katika kuwawezesha kimitaji wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini ili kuwawezesha kuwekeza katika shughuli zao.

Naibu Waziri wa Madini (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa CRDB katika ufunguzi wa mafunzo ya ushirikiano kati ya Wizara ya Madini na Benki ya CRDB uliofanyika Agosti 6, 2020 jijini Dodoma. (Kushoto) ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Prof. Shukrani Manya. (Picha na WM).

Naibu Waziri Nyongo ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo yaliyoandaliwa hususani kwa ajili ya wafanyakazi wa Benki ya CRDB yaliyofanyika katika hoteli na Nashera jijini Dodoma.

Amesema, mafunzo hayo yatawasaidia wataalamu hao wa benki  kuwa na uelewa wa namna shughuli za uchimbaji na biashara ya madini kwa ujumla zinavyoendeshwa.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Prof. Shukrani Manya (wa pili kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa Benki ya CRDB wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya ushirikiano wa Wizara ya Madini na Benki ya CRDB iliyofanyika Agosti 6, 2020  jijini Dodoma, (Picha na WM).

“Biashara ya madini ni kama biashara nyingine, hivyo msisite kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo pindi wanapohitaji kwa ajili ya kuwekeza katika uchimbaji na biashara ya madini,”amesema Nyongo.

Akizungumzia dhumuni la kutoa mafunzo hayo kwa taasisi za benki nchini, ambapo awali mafunzo kama hayo yalitolewa kwa watumishi wa Benki ya NMB, Nyongo amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa Sera ya Madini ya Mwaka 2009 inayoitaka Serikali kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini katika kutatua changamoto za mitaji zinazowakabili na kuwafanya wawekeze kwa tija.

  Baadhi ya wafanyakazi wa CRDB walioshiriki semina hiyo wakifuatilia kwa makini mafunzo ya ushirikiano baina ya benki na Wizara ya Madini uliofunguliwa na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo Agosti 6, 2020 jijini Dodoma. (Picha na WM).

Wizara ikishirikiana na Tume ya Madini imeona njia bora ya kuwawezesha wachimbaji hao ni kuwaunganisha na taasisi muhimu za fedha ili kutoa elimu muhimu kwa taasisi hizo zitakazowasaidia wakati wa kuhakiki taarifa za wachimbaji na wafanyabiashara wa madini pindi watakapowasilisha taarifa zao benki kwa ajili ya kuomba mikopo.

Akizungumzia matarajio ya wizara mara baada ya elimu kutolewa, Nyongo amesema benki zilizopo nchini kuwawezesha kwa kuwapa mikopo na elimu ya biashara wachimbaji wa madini hasa wachimbaji wadogo.

Vilevile Waziri Nyongo amesema, mafunzo hayo yataendelea kutolewa kwa taasisi nyingine za fedha nchini ili kuwezesha taasisi hizo kujifungamanisha kwenye  uchumi wa madini ambayo ni sekta inayoongoza kwa ukuaji nchini.

Akihitimisha hotuba yake ya ufunguzi, Nyongo amesisitiza kuwa elimu ya biashara ya madini itaendelea kutolewa kwa wataalamu wa benki nchini ili kuwajengea uwezo wakopeshaji kutambua fursa zilizopo kwenye sekta ya madini na kuwataka kuajiri wataalamu wenye uelewa na masuala ya madini watakaoweza kuchambua michanganuo ya mikopo ya uchimbaji wa madini vile inavyostahili.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Prof. Shukrani Manya akiwaelezea jambo wafanyakazi wa CRDB walioshiriki mafunzo ya ushirikiano baina ya Wizara ya Madini na sekta za kibenki uliofanyika Agosti 6, 2020 jijini Dodoma. (Picha na WM).

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya amesema, sekta ya madini ni sekta muhimu katika uchumi wa nchi ambayo inahitaji mitaji mikubwa katika uwekezaji wake hivyo ni muhimu kwa watoa huduma za mikopo kuwa na uelewa wa sheria na kanuni za madini.

“Sekta ya madini ni biashara kama biashara nyingine inahitaji mitaji mikubwa hivyo ninyi watu wa benki inabidi mjue vizuri suala la leseni za madini, uhai wa leseni hizo na sheria na kanuni zinazoongoza sekta hii muhimu,”amesema.

Pamoja na hayo, Prof. Manya amesema mafunzo hayo yataondoa kusitasita kutoa mikopo kwa wachimbaji wa madini mara baada ya wataalamu wa mikopo kuwa na uelewa mpana kuhusu mnyororo wa madini unaohusu wachimbaji, wauzaji, vifaa vya uchimbaji na uchakataji wa madini na watoa huduma wengine katika sekta hiyo.

Kwa upande wake, Meneja wa Dawati maalum kwa wateja wakubwa kutoka Benki ya CRDB, Frederick Mwamyalla amekirii kuwa semina hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwao na kuwawezesha kuona fursa zilizopo kwenye sekta ya madini zitakazowasaidia kuongeza mchango wao katika kusukuma mbele ukuaji wa sekta ya madini ili iweze kuchangia vilivyo katika miradi ya maendeleo.

Amesema ni muhimu kwao kama taasisi ya kifedha kuongeza nguvu na kuboresha huduma zao ili kuhakikisha mchango wa benki hiyo unaongezeka kwa kuwawezesha wachimbaji wadogo na hivyo kuinua vipato vyao pamoja na kuongeza mchango wa sekta kwenye pato la taifa.