September 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nyauhenga: Serikali imefanya maboresho makubwa katika miundombinu ya barabara

Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online,

Imeelezwa kuwa katika Serikali ya awamu ya sita,imeongeza fedha za kugharamia ujenzi na matengenezo ya barabara nchini.

Ikiwa njia ya kufanya maboresho katika sekta ya barabara nchini hapa ambayo ndio kiungo kikubwa katika kuchochea maendeleo na uchumi wa taifa.

Hayo yameelezwa na Meneja wa Mfuko wa Barabara Tanzania Bara Eliud Nyauhenga,
wakati akizungumza na ujumbe kutoka Mfuko wa Barabara Zanzibar uliomtembelea ofisini kwake mtaa wa Ammar, jijini Dodoma.

Ambapo ameeleza kuwa kwa miaka yote mitatu iliyopita, Serikali imekuwa ikitoa fedha zote za kugharamia matengenezo ya barabara kama zinavyoidhinishwa na Bunge.

“Hatua hii imewezesha kutekeleza kazi nyingi za matengenezo ya barabara na hivyo kulinda thamani ya uwekezaji wa Serikali kwenye miundombinu yake na kuwawezesha watumiaji wengi wa barabara kupata huduma nzuri za usafiri na usafirishaji.,”

Ameeleza kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imefanya maboresho ya barabara ambapo,kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 imekuwa ilitenga kiasi bilioni 440 kila mwaka kwa ajili ya kuboresha miundombinu hiyo ya mijini na vijijini.

Hatua hiyo imefanya kuimarika kwa kiwango kikubwa cha mtandao wa barabara za vijijini ikiwa ni pamoja na kufungua barabara nyingi ambazo zilikuwa hazipitiki hapo awali.

“Maboresha haya yanawawezesha wananchi kufikia na kunufaika na huduma za kijamii na kiuchumi zinazopatikana kutokana na miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali ,” ameeleza Nyauhenga.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa makusanyo ya fedha za kugharamia matengenezo ya barabara yameongezeka kwa asilimia 27 kutoka bilioni 806.7 mwaka wa fedha 2019/20 hadi bilioni 1,027 mwaka wa fedha 2021/22.

Ametumia fursa hiyo kueleza kuwa serikali ilianzisha Mfuko wa Barabara Tanzania mwaka 2000 kupitia Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta Sura ya 220 ili kugharamia kikamilifu matengenezo ya barabara zote za Tanzania Bara.

“Chanzo kikuu cha mapato ya mfuko huo ni tozo za mafuta, kiasi cha shilingi 363 kwa kila lita ya dizeli na petrol huku vyanzo vingine ni tozo kwa magari ya kigeni yanayotumia barabara nchini pamoja na faini zinazotozwa kutokana na uzidishaji uzito wa magari.,”ameeleza Nyauhenga.

Vilevile amewaasa wananchi kutunza miundombinu ya barabara kwenye maeneo yao ikiwa ni pamoja na kuzilinda samani za barabara, kutotupa takataka kwenye mifereji ya barabara, kutokutiririsha maji na kutopitisha mifugo barabarani.

Kwani serikali imewekeza fedha nyingi kwenye miundombinu ya barabara na pia ndiyo njia ya usafiri na usafirishaji inayotumiwa zaidi hapa nchini,hivyo uharibifu wake huleta hasara kubwa na kuwafanya wanachi wengi kukosa huduma za usafiri na usafirishaji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kuandaa Muongozo wa Utumiaji Barabara Zanzibar, CPA Bakari Rashid, ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeunda Kamati hiyo ili kuboresha matumizi ya barabara za Zanzibar.

Ambapo Kamati yake tayari imetembelea barabara zote za Unguja na Pemba kabla ya kuamua kutembelea Mfuko wa Barabara Tanzania Bara.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Mapitio ya Mpango Mkakati wa Mfuko wa Barabara Zanzibar, Omar Makame ameeleza kuwa kamati zao zimejifunza mambo mengi kuhusu uendeshaji wa Mfuko wa Barabara hivyo mfuko wao utaendeleza ushirikiano madhubuti uliopo baina ya Mifuko hiyo miwili nchini.

Kamati ya Kuandaa Mwongozo wa Utumiaji Barabara Zanzibar pamoja na Kamati ya Mapitio ya Mpango Mkakati wa Mfuko wa Barabara Zanzibar zipo mkoani Dodoma kwa ziara ya siku mbili, ili kujifunza na kujionea utendaji kazi wa Mfuko wa Barabara Tanzania Bara.

Meneja wa Mfuko wa Barabara Tanzania Bara Eliud Nyauhenga akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Kuandaa Mwongozo wa Utumiaji Barabara Zanzibar pamoja na Kamati ya Mapitio ya Mpango Mkakati wa Mfuko wa Barabara Zanzibar (hawapo pichani) walipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma.
Wajumbe wa Kamati ya Kuandaa Mwongozo wa Utumiaji Barabara Zanzibar pamoja na Kamati ya Mapitio ya Mpango Mkakati wa Mfuko wa Barabara Zanzibar wakimsikiliza Meneja wa Mfuko wa Barabara Tanzania Bara Eliud Nyauhenga (hayupo pichani), walipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma.