November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Mwanza Emmanuel Kahensa akimkabidhi barakoa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza Edwin Soko,ambapo NSSF kupitai meneja wake wametoa msaada wa barakoa 200 kwa waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza ili waweze kutimiza majukumu yao wakiwa wamejikinga na maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na kirusi aina ya Corona (COVID-19). Picha na Judith Ferdinand.

NSSF yasaidia waandishi wa habari

Na Judith Ferdinand,Mwanza

MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Mwanza umetoa msaada wa barakoa zaidi ya 200 kwa waandishi wa habari ili ziweze kuwasaidia kujikinga na ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) wakati wakitimiza majukumu yao ya kila siku mkoani hapa.

Aidha, pia wadau wengine ndani na nje ya mkoa huo wamehimizwa kujitokeza zaidi kusaidia kundi hilo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya msaada huo kwa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), Meneja wa NSSF Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Kahensa amesema katika kutambua umuhimu na kuthamini mchango wa sekta ya afya na waandishi wa habari ndio maana wameguswa kwa kutoa barakoa hizo kwa kundi hilo.

Kahesa amesema, ni ili kundi hilo liweze kutimiza majukumu ya kuhabarisha umma wakiwa salama katika kipindi  hiki cha mapambano dhidi ya corona.

Pia amewahamasisha wadau mbalimbali waliopo mkoani humo kusaidia MPC ili waweze kupata vifaa ambavyo ni barakoa zinazotakiwa kutumiwa tatu kwa siku na vitakasa mikono (sanitizer) watakazokuwa wanatembea nazo wakati wa majukumu yao.
“Katika mapambano ya corona NSSF tunathamini mchango wao pamoja na wenu nyinyi waandishi wa habari ambao mmekuwa mkifanya kazi ya kuelimisha watu kuhusiana na hili janga,na wanachama wetu ambao tunawahimiza kuvaa barakoa pia wanaweza kupata huduma bila kufika ofisini kwa njia ya simu,tumeguswa kuwachangia barakoa nyinyi waandishi ili mzitumie katika kazi zenu,”amesema Kahensa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa MPC, Edwin Soko ameishukuru NSSF kwa msaada wao kujitolea kuwasaidia waandishi wa habari mkoani humo kwa ajili ya kuwakinga na ugonjwa huo ambao wapo zaidi ya 200, kwani wanafanya katika mazingira hatarishi ukiondoa kundi la sekta ya afya, kwani wao wanafanya kazi saa 24 kwa ajili ya kuelimisha jamii.

“NSSF imejitoa kuhakikisha waandishi tunakuwa salama katika mkutadha huu wa mapambano dhidi ya corona wakati wa kazi zao na changamoto zipo nyingi katika sekta hii,waandishi wa habari wote watapatiwa barakoa hizo na ni wapongeze waandishi wa habari kwa kufanya kazi, hivyo niwaombe muendelee kufanya kazi kwa kufuata misingi ya taaluma zetu,”amesema Soko.