January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NSSF yakutana na wahariri nchini

*Yatambulisha Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya Sekta Isiyo Rasmi (NISS)

*Sasa mwanachama kufungua madai ya mafao kidijitali ‘online’

*Yaweka kipaumbele cha matumizi ya TEHAMA, zaidi ya asilimia 82% sasa zinafanyika kutumia mifumo

* Yatoa Tuzo kwa Vyombo vya Habari vinavyotekeleza vyema sheria ya NSSF, yatambua mchango wa wahariri wastaafu

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Masha Mshomba ameanika mafanikio mbalimbali ambayo Mfuko umeyafanya yenye lengo la kumuondolea kero mwanachama na kumsogezea huduma huko huko aliko kwa kutumia mifumo ya TEHAMA. Pia ametambulisha Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Sekta isiyo rasmi (NISS).

Bw. Mshomba ameeleza mafanikio hayo tarehe 1 Oktoba 2024 wakati akifungua mkutano wa NSSF na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ulioshirikisha wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari Nchini, uliofanyika katika ukumbi wa NSSF Mafao House Ilala, Dar es Salaam.

Amesema wanaipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo amekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya NSSF hasa katika miaka minne iliyopita ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa la waajiri na wanachama katika Mfuko tofauti na kipindi cha nyuma na kupelekea thamani ya Mfuko kufikia trilioni 8.5 tofauti na trilioni 4.8 wakati alipokuwa anaingia madarakani. 

Bw. Mshomba amesema NSSF inaendelea kuboresha huduma zake kupitia mifumo ya TEHAMA na sasa shughuli nyingi za NSSF zinafanyika kupitia mifumo na kuwa mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa fedha 2024/25, huduma zote muhimu zitatolewa kupitia mifumo, aidha alifafanua ya kwamba kwa sasa zaidi ya asilimia 80 ya shughuli za Mfuko zinafanyika katika Mifumo tofauti na asilimia 42 ya mwaka 2021/22

“Kupitia mifumo ya TEHAMA, NSSF imeweza kuwafikia kwa ukaribu wanachama na wadau wake ambapo kwa sasa hawalazimika kufuata huduma ofisini badala yake wanazipata huko huko waliko na hivyo tumewaondolea adha ya kufuata huduma umbali mrefu,” amesema Bw. Mshomba.

Aidha, amesema NSSF imezindua mfumo unaomuwezesha mwanachama kufungua madai ya mafao kwa njia ya mtandao na kuwa lengo ni kumrahisishia mwanachama kupata huduma karibu zaidi bila ya kufika katika ofisi za NSSF. Pia Mfumo huu utaondoa kabisa usumbufu kama ulikuwepo na pia utawawezesha wanachama wetu tunaowahudumia kupata huduma kwa wakati, kwa kuwa mifumo hii ni wazi na ufuatiliaji unakuwa rahisi.

Kuhusu sekta isiyo rasmi, Bw. Mshomba amesema Mfuko umechukua hatua mbalimbali kuhakikisha wananchi wengi wanahamasika kujiunga na kujiwekea akiba, ambapo kwa sasa unaendelea kutoa elimu kupitia makundi mbalimbali na kuwaeleza faida za kujiwekea akiba kwa maisha ya sasa na ya baadaye.

Aidha, kuanza kwa Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Sekta isiyo rasmi (NISS), ni utekelezaji wa mipango mahsusi iliyowekwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) (Millenium Goals) ambayo pamoja na mambo mengine inataka watu wote kuwa kwenye hifadhi ya jamii. Mshomba alifafanua kuwa NSSF imeshaweka mikakati ya kutosha kuwafikia watu wote ikiwa ni kwa makundi na hata mwananchi mmoja mmoja. Wananchi wote watakaojiunga na NSSF watapata Mafao na Huduma mbalimbali kama ambavyo wafanyakazi wengine wote wanapata.

Uwepo wa Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Sekta isiyo rasmi (NISS) utatoa fursa ya kuongeza wigo wa Hifadhi ya Jamii kwa makundi ambayo hayanufaiki na huduma hizi ingawa wanashiriki kikamilifu kuchangia uchumi wa nchi, utasaidia juhudi za Serikali za kupunguza umaskini wa kipato kwa wananchi, utaongeza nguvu za uzalishaji mali na kukuza uchumi wa Nchi na mwisho utachochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Bw. Mshomba amesema pia NSSF ina Skimu ya uchangiaji wa Hiari ambayo inawahusu watumishi wote. “Natumia nafasi hii kuhamasisha na kuwataka mchangie kupitia skimu hii kwa sababu kufanya hivyo mtajikuta mnapata kipato cha ziada, kazi kubwa mbele yetu ni kutoa elimu ili watu wengi wapate uelewa wa jambo hili.” amesema.

Naye, Mwenyekiti wa  Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amepongeza mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na NSSF hasa katika kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ukiwemo wa kukamilisha kiwanda cha sukari Mkulazi. Pia amepongeza NSSF kuweka mipango sasa ya kuwafikia wananchi wote walioko katika Sekta isiyo rasmi kwani kwa kufanya hivyo sasa watu wote tutakuwa ni wamoja na hapo baadaye wote tutanufaika, safari ya uzee ni ya kila mmoja wetu na hivyo ni vizuri kila mmoja akifika awe na uhakika wa kesho yake.

Balile alitumia fursa hiyo kuwakumbusha waajiri wa sekta binafsi hasa wamiliki wa vyombo vya habari kuhakikisha wanawasilisha michango ya wafanyakazi wao NSSF kwa wakati ili wanapostaafu waweze kulipa stahiki zao. 

“Leo tumepata bahati tumepata ushuhuda kutoka kwa wastaafu waliokuwa wafanyakazi kutoka katika vyombo vya habari ambao ni wanufaika wa mafao ya kustaafu na pensheni ya kila mwezi Bi. Flora Wingia na Bw. Bakari Machumu” Aidha, wahariri wastaafu wamepewa Tuzo kwa kutambua mchango wao.

Akiwasilisha taarifa ya uendeshaji wa Mfuko, Mkurugenzi wa Uendeshaji, Bw. Omary Mziya amesema NSSF inaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ambayo ni kuandikisha wanachama kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao.

Bw. Mziya amesema wanaendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa hifadhi ya jamii ili kuongeza uelewa wa haki ya kujiunga kwenye Skimu ya Hifadhi ya Jamii kwa Sekta isiyo rasmi  (NISS) na kuendelea kuboresha mifumo na kusogeza huduma karibu na jamii.

“Sekta isiyo rasmi ina Watanzania takribani 11 Millioni, hawa wote wanahitaji kinga dhidi ya majanga ambayo ni uzee na majanga mengine yanayoweza kutokea hapa kati, kuachishwa kazi ama kufariki na kadhalika”. 

Sekta isiyo rasmi inatoa nafasi kwa Watanzania wote kujiunga na hifadhi ya jamii, Mwananchi yeyote aliyejiajiri katika sekta isiyo rasmi kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji mdogo wa madini, sanaa mbalimbali, biashara ndogo ndogo, mama lishe/ Baba lishe, bodaboda na wasafirishaji wengine, machinga, wanahabari wa kujitegemea.