December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, William Erio.

NSSF yaanika mafanikio matatu muhimu matumizi ya GePG

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAKATI Serikali kupitia Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James,  ikisema kuwa mfumo wa Kielektroniki wa malipo Serikalini (GePG) umesaidia kuongeza makusanyo kwa asilimia 292, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limeainisha maeneo matatu makubwa yaliyofanikiwa kutokana na matumizi ya mfumo huo ikiwemo ukubwa wa Shirika kukua.

Hayo yalisemwa Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, William Erio, wakati wa mkutano wa kupokea ripoti ya tathimini ya mfumo wa GePG, kuwa kutokana na matumizi ya mfumo huo ukubwa wa Shirika hilo umekuwa kutoka sh. Trilioni 3.2 hadi kufikia sh. trilioni 4.4.

Aidha, alisema makusanyo ya michango kutoka kwa wanachama nayo yameongezeka kutoka sh. bilioni 694 kwa mwaka na kufikia Shilingi Trilioni 1.1 hadi kufikia Juni mwaka huu.

Erio alisema mfumo huo ambao ulianza kutumia rasmi katika Shirika hilo mwezi Aprili mwaka jana, umesaidia kuongeza mapato, kupunguza gharama za uendeshaji walizokuwa wanazitumia katika matumizi ya kawaida na kuwawezesha kutoa huduma bora zaidi kwa wanachama na kwa wakati.

Alisema NSSF inautumia mfumo huo kukusanya michango kwa wanachama kutoka sekta rasmi na sekta isiyo rasmi pamoja na kukusanya kodi ya pango kwa wapangaji waliopanga kwenye vitenga uchumi vya Shirika hilo.

Erio alisema matumizi ya mfumo huo yamesaidia Shirika hilo kuondoa hudi hewa za malipo, ambapo kipindi cha awali kulikuwa na hundi hewa nyingi ambazo zilikuwa zinaondoa weledi wa kazi katika Shirika hilo, na kwamba kabla ya mfumo huo kulikuwa na akaunti za benki 78, lakini baada ya mfumo huu tumeondoa akaunti na kubaki na akaunti 3 tu.

“Hii GePG imeleta mabadiliko makubwa NSSF, imeongeza thamani ya mfuko kwa zaidi ya asilimia 40 ndani ya kipindi cha miaka miwili ni kutokana na matumizi ya mfumo huu,” alisema Erio.

Awali, Doto aliipongeza NSSF kwa kuongeza ukubwa wa Shirika pamoja na kuongeza makusanyo kutokana na kutumia mfumo huo wa GePG, na kwamba Shirika hilo liwe mfano wa kuigwa kwa mashirika mengine ya umma na taasisi za Serikali.

“Kama alivyosema Mkurugenzi Mkuu wa NSSF (William Erio) huo ni ushuhuda tosha kwani unaweza ukaona thamani ya Shirika imepanda sana kutokana na matumizi ya GePG,” alisema Doto.

Alisema thamani ya NSSF ndani ya miaka miwili baada ya kutumia mfumo wa GePG, imeongezeka, makusanyo yamepanda sana na kwamba Shirika akanti nyingi zilizokuwa zinatumika awali ndivyo sivyo zimefungwa.

“Huu ndio uwe mfano wa kuigwa na mashirika mengine yote yaliyobaki…sisi kama Serikali tunaipongeza sana NSSF kwa mafanikio haya makubwa ndani ya kipindi kifupi,” alisema Doto.

Doto alisema mfumo huo ndani ya Serikali umeleta mafanikio makubwa ikiwemo kuongeza kiwango cha makusanyo tangu ulipoanzishwa mwaka 2017, kwani takwimu za maduhuli yaliyokusanywa mwaka wa fedha 2015/16, Serikali ilikuwa inakusanya kwa mwaka maduhuli ya sh. bilioni 688.7, lakini katika mwaka wa fedha 2019/2020, makusanyo yamefikia sh. trilioni 2.699.

“Ukiangalia mwaka wa fedha 2015/16 na 2019/20, tumeongeza ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa asilimia 292 kiasi ambacho ni kikubwa sana,” alisema Doto.