March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NPC yawanoa maafisa Mipango nchini

Na Joyce Kasiki, Dodoma

SERIKALI  imeanza mchakato mpya wa kuimarisha mfumo wa kupanga maendeleo nchini kwa kutoa mafunzo maalumu kwa wataalamu wa mipango na uchumi kutoka wizara, mikoa na halmashauri zote, ili kuhakikisha utekelezaji thabiti wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unaanza kwa kasi na kwa weledi.

Hatua hiyo imebainishwa jijini Dodoma na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango (NPC), Dkt. Fred Msemwa, alipofungua warsha ya siku mbili iliyowakutanisha Wakurugenzi wa Mipango na Sera, Wakuu wa Idara za Uchumi, wataalamu wa Mahakama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na taasisi nyingine za umma.

Dkt. Msemwa alisema Serikali inajenga misingi mipya ya kupanga maendeleo kupitia mwongozo maalumu unaoandaliwa kwa ajili ya kuwezesha taasisi zote za umma kutayarisha mipango mikakati yenye mwelekeo mmoja na inayohusiana moja kwa moja na Dira 2050.

“Tunataka kila sekta iwe na mpango mkakati unaokidhi vigezo vya kitaifa na unaoelekeza moja kwa moja katika malengo ya Dira 2050. Ndiyo maana mafunzo haya ni muhimu yanatoa dira, mwongozo na taratibu sahihi za kupanga,” alisema Dkt.Msemwq

Akizungumzia tathmini ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2025, Dkt. Msemwa alisema hadi sasa taifa limepiga hatua kubwa katika sekta za elimu, afya, miundombinu na hifadhi ya jamii, ingawa changamoto kadhaa zimeendelea kushuhudiwa katika maeneo mengine.

Alisema Rasimu ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2025/26–2029/30), ambao ni sehemu ya utekelezaji wa Dira 2050, imewasilishwa kwa washiriki wa mafunzo ili kutoa fursa ya kupokea maoni na marekebisho kabla ya kuwasilishwa serikalini kwa hatua zaidi.

“Haya mafunzo ni jukwaa la kuanzia safari ya kupata mpango wenye uhalisia, unaoweza kutekelezeka na unaoendana na matarajio ya wananchi. Tunahitaji mawazo ya wataalamu hawa ili kuhakikisha tunaboresha pale ambapo hapakufanya vizuri,” alisisitiza.

Kwa upande wao, washiriki wa warsha hiyo waliipongeza Serikali kwa hatua ya kutoa mafunzo mapema kabla ya kuanza rasmi kwa utekelezaji wa Dira 2050.

Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tunduma, Innocent Maduhu, alisema mafunzo hayo yameleta mwanga mpya kuhusu namna taasisi zinavyopaswa kusimamia maendeleo.

“Dira bila mpango ni kama ramani isiyo na mwelekeo. Tunampongeza Rais Dk. Samia kwa kutuletea dira iliyo wazi na inayoonesha mustakabali wa taifa. Tukitekeleza kama ilivyoelekezwa, hakuna atakayebaki nyuma kwenye maendeleo,” alisema.

Naye Katibu Tawala Msaidizi wa Mipango na Uratibu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Edina Katakaiya, alisema mpango wa miaka mitano uliowasilishwa katika warsha hiyo unazungumzia matokeo yanayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

“Tunachoangalia sasa ni mpango unaoonekana kwa wananchi, sio maneno kwenye makaratasi. Ndiyo maana ushirikishwaji wa wataalamu katika hatua hizi za awali ni muhimu,” alisema.